Na INSP. Nurdini Nanyanga – DSM

Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu, leo Agosti 13, 2026, amefanya ziara katika Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China, jijini Dar Es Salaam na kukutana na Balozi wa nchi hiyo hapa Tanzania Mhe. Chen Mingjian.

Katika ziara hiyo, CGP Katungu amesema lengo ni kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Magereza na China, hususan katika maeneo ya teknolojia na kilimo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Jeshi la Magereza kuongeza uzalishaji na kujitosheleza kwa chakula.

Amesema Jeshi la Magereza liko tayari kushirikiana na kampuni na wadau mbalimbali katika uwekezaji, kwa kuzingatia sheria, taratibu na maslahi ya pande zote.

Kwa upande wake, Mhe. Chen Mingjian, amesema Tanzania na China zimekuwa na ushirikiano mzuri, huku kampuni nyingi za China zikionyesha nia ya kuwekeza nchini. Ameahidi kuyapa kipaumbele mazungumzo yao na kuendelea kubadilishana taarifa na Jeshi la Magereza ili kutafuta fursa za ushirikiano katika teknolojia na sekta ya kilimo.