Mkurugenzi wa Kampuni ya Farmtech Solutions inayojihusisha na uuzaji wa matrekta ya Zoomlion, mashine na vifaa bora vya kilimo,Injinia Assey Deogratius akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya nanenane Themi,Njiro.


…………
Na Happy Lazaro, Arusha.
WAKULIMA nchini wametakiwa kuendelea kutumia teknolojia ya mashine za kisasa za kilimo ili kuongeza tija, kupunguza gharama za uzalishaji na kurahisisha shughuli mbalimbali za kilimo.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Farmtech Solutions inayojihusisha na uuzaji wa matrekta ya Zoomlion, mashine na vifaa bora vya kilimo,Injinia Assey Deogratius wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya nanenane Themi,Njiro.
Injinia Assey amesema kuwa , kampuni hiyo ambayo ni wakala wa matrekta ya Zoomlion katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida na Dodoma, dhamira yake kubwa ni kuwafikishia wakulima teknolojia za kisasa za kilimo.
“Sisi kazi yetu ni moja tu kugawia kila mkulima trekta na tunatoa suluhisho za kisasa za vifaa vya kilimo kwa wakulima na wawekezaji wa sekta ya kilimo,ambapo pia tunaagiza vifaa na spare za vifaa vya kilimo kutoka China na kuvisambazaTanzania kwa bei nafuu.”amesema Injinia Assey .
“Wakulima wetu wanapaswa kujua kuwa spare za trekta zetu zinapatikana hapa hapa nchini Tanzania kwani kiwanda kipo jijini Dar es Saalam ,na kwa upande wa matrekta ya Zoomlion wanazo 50 HP, 70 hp, 75 HP, 90 Hp ,130 Hp na tairi zote nne ni (4WD) na zina matumizi madogo sana ya mafuta (lita 2.5 hadi lita 5) na zina uwezo mkubwa wa kuvuta tela”amesema Injinia Assey.
Amesema kuwa,Farmtech Solutions haitoi matrekta pekee, bali inashughulikia mnyororo mzima wa shughuli za kilimo kuanzia uandaaji wa mashamba, kulima, kupanda, kupalilia, kuvuna hadi uchakataji wa mazao, hatua ambazo zote zinaweza kurahisishwa kwa matumizi ya mashine sahihi.
“Wakulima wengi bado wanaamini trekta hutumika kwa shughuli ya kulima pekee, wakati ukweli ni kwamba linaweza kutumika pia kupanda, kupalilia, kuvuna, kusafirisha mazao na kuendesha vifaa mbalimbali vinavyorahisisha kazi za shambani na ndio upekee mkubwa wa matrekta yetu ya Zoomlion “amesema
Ameongeza kuwa, pamoja na matrekta, kampuni hiyo pia ina mashine nyingine zikiwemo doza zinazotumika kusafisha mashamba kabla ya kuanza shughuli za uzalishaji, huku wataalamu wao wakiendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mashine hizo ili kuongeza ufanisi.
Injinia Assey ameongeza kuwa, teknolojia ya matrekta ya Zoomlion imeundwa kwa kuzingatia urahisi wa matumizi, hivyo inaweza kuendeshwa na vijana, wanawake na hata wazee, jambo linalopunguza utegemezi wa nguvu kazi nyingi na gharama kubwa za uzalishaji.
“kupitia ushiriki wetu katika Maonesho ya Nanenane, Farmtech Solution inalenga kuwajengea wakulima uelewa kwamba uwekezaji katika mashine za kisasa si anasa, bali ni njia muhimu ya kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama na kuifanya sekta ya kilimo kuwa yenye faida zaidi.”amesema Injinia Assey.
Aidha amewataka wakulima kutumia vifaa vya kampuni hiyo kwani wanawasaidia kupata vifaa vya kilimo kwa bei nzuri moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji nchini China ambapo pia wanatoa ushauri wa kitaalamu kwa kuwasaidia wakulima kuchagua vifaa vinavyofaa kulingana na aina ya shughuli za kilimo na bajeti yake.
