Na Mwandishi wetu, Simanjiro. 

AFISA usafirishaji (TO) wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Ismail Khalfan Ismail amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya shilingi milioni 1 na mahakama ya Wilaya ya Simanjiro kwa wizi wa betri mbili za gari.

Ismail ametiwa hatiani Agosti 7, 2026, mbele ya Hakimu mkazi mkuu mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro Charles Uisso, mji mdogo wa Orkesumet.

Hakimu Uisso amesema Ismail ametiwa hatiani katika shauri la jinai namba 7118/2026 lililoendeshwa na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Simanjiro, Faustin Mushi.

“Mshtakiwa hapo awali alikuwa anashtakiwa kwa kosa la wizi akiwa mtumishi wa umma kinyume na k/f cha 258(1), 265 na 270 vya sheria ya kanuni ya adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023,” amesema hakimu Uisso.

Amesema mshtakiwa alifanya kosa hilo kwa kuiba betri mbili zenye thamani ya shilingi 500,000 za magari ambayo ni mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.

Amesema mshtakiwa huyo alizinunua kwa fefha alizokuwa amepewa na mwajiri wake ambaye ni Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.

Ameeleza kwamba mshtakiwa huyo ametiwa hatiani na kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani.

Hata hivyo, amesema mshtakiwa huyo alipe faini ya shilingi 500,000 kwa mahakama pamoja na fidia ya shilingi 500,000 kwa mwajiri wake ambaye ni Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro