Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga akipata maelezo kuhusu huduma zinazotolewa na benki hiyo kutoka kwa Meneja wa tawi  la Azania benki Ambokile Tuntufye katika maonesho ya nanenane Njiro.
Afisa Mahusiano wa benki ya  Azania tawi la Arusha, Winnifrida Mwacha, akimkabithi zawadi Mkuu wa wilaya ya Manyara mara baada ya kutembelea banda hilo
…………
Na Happy Lazaro, Arusha.
Wanawake nchini wamehimizwa kutumia fursa za huduma za kifedha zinazotolewa na  benki ya Azania  kupitia akaunti maalumu ya “Fanikisha Wewe, ni hodari” inayolenga kuwawezesha wanawake wajasiriamali, wafanyabiashara, wakulima na wafugaji kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Akitoa maelezo hayo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Manyara Quen Sendiga mara baada ya kutembelea   maonesho hayo  Afisa Mahusiano wa benki ya  Azania tawi la Arusha, Winnifrida Mwacha, amesema benki hiyo inatoa elimu ya kifedha kwa makundi mbalimbali ikiwemo wakulima, wanawake, wanafunzi na wafanyabiashara ili kuwajengea uwezo wa kutumia huduma za kifedha kwa maendeleo yao.
Mwacha  amesema akaunti ya “Fanikisha Wewe” imebuniwa mahsusi kwa ajili ya wanawake na inafunguliwa bila malipo, haina makato ya kila mwezi na humwezesha mteja kupata kadi ya Visa pamoja na huduma za kidijitali za Azania Mobile Banking na Azania Lipa kwa urahisi wa kufanya miamala.
Ameongeza  kuwa, kupitia akaunti hiyo, wanawake wanaweza kupata mikopo yenye riba nafuu ya asilimia moja, kuanzia shilingi 200,000 hadi milioni 500 kulingana na uwezo wa biashara na kipato cha mwombaji.
Mwacha  kuwa, wanawake wanaostahili kupata huduma hiyo ni wale wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi kama biashara, kilimo au ufugaji, wenye biashara zilizosajiliwa na kutimiza masharti ya msingi ikiwemo kuwa na akaunti ya Fanikisha Wewe.
Amefafanua kuwa, hata wanawake ambao hawana biashara zilizosajiliwa wanaweza kunufaika kupitia vikundi, ambapo benki ya  Azania pia inatoa mikopo kwa vikundi vya wanawake vinavyokidhi vigezo vilivyowekwa.
Mwacha amewataka wanawake kote nchini kutembelea matawi ya  benki ya Azania au banda la benki hiyo katika Maonesho ya Nanenane ili kupata elimu zaidi na kufungua akaunti zitakazowawezesha kupata huduma mbalimbali za kifedha na fursa za kukuza uchumi wao.
Akizungumzia upande wa akaunti ya wanafunzi amewataka wanafunzi kufungua akaunti mapema ili kunufaika na “Boom advance “
Aidha amewahimiza wanafunzi wanaotembelea Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini kufika katika banda la benki hiyo ili kupata elimu ya kifedha na kufungua akaunti maalumu  za wanafunzi zitakazowawezesha kujenga utamaduni wa kuweka akiba tangu wakiwa wadogo.
 Amesema kuwa ,akaunti ya mwanafunzi inafunguliwa bila malipo na haina makato ya kila mwezi, hivyo kumwezesha mwanafunzi kuweka akiba kwa urahisi.
Ameongeza kuwa, akaunti hiyo inawafaa wanafunzi wa shule za sekondari na itaendelea kuwahudumia hata watakapojiunga na vyuo vya elimu ya juu.
“Benki ya Azania  ina huduma ya Boom Advance, inayomwezesha mwanafunzi wa elimu ya juu kupata fedha za mkopo wa elimu (boom) kupitia simu yake ya mkononi akiwa chuoni au hostel bila kulazimika kufika tawi la benki.”amesema
Mwacha amefafanua kuwa, wanafunzi wanaofungua akaunti hiyo hupatiwa kadi ya ATM pamoja na huduma nyingine za benki zinazowawezesha kufanya miamala kwa urahisi na usalama zaidi.
Amewataka  wanafunzi kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea banda la Benki ya  Azania ili kupata elimu ya matumizi sahihi ya huduma za kifedha, kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kujifunza namna bora ya kusimamia fedha zao mapema.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Manyara,Queen Sendiga akizungumza katika banda hilo ameipongeza benki hiyo kwa namna ambavyo inatoa huduma nzuri kwa wananchi hususani mikopo nafuu yenye riba nafuu na kuwawezesha wanawake wote kumudu gharama hizo.
“Tumekuwa tukizielekeza taasisi za kifedha zinazofanya kazi katika Kanda ya Kaskazini kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, hususani wakulima, wafugaji na wavuvi ambao wengi wao wanaishi maeneo ya vijijini na pembezoni na nimefurahi kuona benki hii inatekeleza agizo hilo.”amesema Sendiga.
Sendiga amesema kuwa ,ni muhimu kuwafikia wananchi  wakiwa kwenye maeneo yao na kuwaeleza namna wanavyoweza kupata mikopo nafuu itakayowasaidia kukuza shughuli zao za kilimo, ufugaji na uvuvi.
“Tunawasihi wananchi wasisite kutembelea mabanda ya taasisi hizi. Wasiende tu kuangalia bidhaa na maonesho mengine, bali watenge muda wa kupita kwenye taasisi hizi za fedha ili kupata elimu kuhusu huduma za kifedha zinazotolewa.”amesema 
“Tunawakaribisha wakulima, wafugaji, wavuvi na Watanzania wote kutembelea Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini ili wapate elimu, huduma za kifedha na fursa zitakazowawezesha kuongeza mitaji, kukuza biashara zao na kuinua uchumi wao.”amesema