NAIBU WAZIRI wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray, amemtaka mkandarasi wa mradi wa Mikocheni Apartments kuongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo Oktoba mwaka huu.

Mhe. Qwaray ametoa maelekezo hayo leo, Agosti 7, 2026, alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo jijini Dar es Salaam, unaosimamiwa na kumilikiwa na Watumishi Housing Investments (WHI).

Aidha, amemtaka mkandarasi kuongeza nguvu zaidi katika utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kuwawezesha watumishi wa umma ambao tayari wamelipia nyumba hizo kuhamia mara utakapokamilika.

Pia, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora wa ujenzi ili nyumba zinazojengwa zidumu kwa muda mrefu na Serikali iweze kuona thamani ya fedha iliyowekezwa.

Sambamba na hilo, Naibu Waziri huyo ametoa wito kwa watumishi wa umma na wananchi wenye sifa kujiunga na Mfuko wa Faida Fund ili kujenga akiba ya muda mrefu itakayowawezesha kuwa na uhakika wa kifedha baadaye.

Amesema kujiunga na mfuko huo kutawasaidia watumishi wa umma kuongeza mafao yao ya uzeeni bila kuathiri mafao ya msingi yanayolipwa kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii, huku akisisitiza kuwa uwekezaji wa mapema ni msingi wa ustawi wa kifedha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investments (WHI), Sephania Solomon, amesema taasisi hiyo inatekeleza mradi wa nyumba 101 katika eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam, ambapo kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 80.

“Mkandarasi anatakiwa kukamilisha ujenzi wa nyumba hizi ifikapo mwisho wa Oktoba 2026 ili wanunuzi waanze kunufaika kwa kuhamia na kuanza kuishi,” alisema Solomon.

Aliongeza kuwa maelekezo yaliyotolewa na Naibu Waziri wameyapokea na wataendelea kumsimamia mkandarasi ili ahakikishe anakamilisha mradi huo kwa wakati kama mkataba unavyoelekeza.

“Sisi maelekezo ya Waziri tumeyapokea na tutaendelea kumsimamia mkandarasi ili aweze kukamilisha nyumba hizi kwa wakati, kama mkataba unavyotaka,” alisema.

Solomon amesema mkandarasi alianza utekelezaji wa mradi huo mwezi Septemba 2024 kwa mkataba wa miezi 18, huku thamani ya mradi ikiwa shilingi bilioni 18 pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Alibainisha kuwa nyumba zote zimeuzwa kwa watumishi wa umma.

“Gharama za kununua nyumba hizi ni ndogo kwa zaidi ya asilimia 30 ukilinganisha na bei ya soko. Ukifanya ulinganisho wa thamani ya nyumba katika eneo hili, utabaini kuwa bei zetu ni nafuu na zimekusudiwa kuwahudumia watumishi wa umma,” alisema.

Aidha, amesema wanunuzi wote wa nyumba hizo tayari wamepatikana na kilichobaki ni kukamilisha ujenzi na kuzikabidhi kwa wamiliki wake.

Amewataka wanunuzi ambao bado hawajakamilisha malipo yao kufanya hivyo kwa wakati, kwa kuwa mkataba unawataka wawe wamekamilisha malipo ifikapo wakati wa kukabidhiwa nyumba.

“Kwa sasa wanunuzi wanatakiwa kukamilisha malipo ya mwisho. Nyumba zote 101 tayari zimeshauzwa kwa watumishi wa umma,” alisema Solomon