Afisa Mazingira wa kampuni hiyo,Getruda Salingo akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja Themi, Njiro mkoani Arusha.
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha .Kampuni ya ununuzi wa zao la parachichi aina ya Hass na Fuerte ya AVOAfrica imewataka wakulima katika maeneo yenye hali ya hewa ya baridi kuongeza uzalishaji wa parachichi aina ya Hass (Upele) kwani soko lake ni la uhakika nje ya nchi .
Aidha imeelezwa kuwa ,zao hilo la parachichi linaendelea kupata mahitaji makubwa katika masoko ya kimataifa na kuwapa wakulima fursa ya kuongeza kipato.
Hayo yamesemwa na Afisa Mazingira wa kampuni hiyo,Getruda Salingo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja Themi, Njiro mkoani Arusha.
Getruda amesema kuwa, AVOAfrica imeshiriki maonesho hayo kwa lengo la kuwafikia wakulima, kutoa elimu kuhusu kilimo cha parachichi aina ya Hass na kuwahakikishia soko la uhakika kwa mazao yao.
Amesema kampuni hiyo, yenye makao yake mkoani Njombe, inajishughulisha na ununuzi wa parachichi kutoka kwa wakulima na kwa sasa inakusanya mazao hayo katika mikoa ya Njombe, Mbeya, Iringa na Ruvuma, huku ikitarajia kupanua shughuli zake hadi mkoani Arusha kutokana na mwitikio mkubwa wa wakulima.
“parachichi aina ya Hass ndiyo inayohitajika zaidi katika masoko ya nje kwa sababu ina kiwango kikubwa cha mafuta na ubora unaokidhi mahitaji ya wanunuzi wa kimataifa. .”amesema .
Amebainisha kuwa kwa sasa kampuni hiyo inauza zaidi katika masoko ya Saudi Arabia na Dubai ambapo mahitaji ni makubwa sana hivyo wakulima wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo ambayo soko lake ni la uhakika .”amesema Getruda.
“wakulima wengi wa Arusha wameonyesha nia ya kuingia katika kilimo hicho, lakini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa soko la uhakika hivyo kutokana na hali hiyo, AVO Africa inapanga kufungua ofisi mkoani Arusha ili kurahisisha huduma kwa wakulima na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mazao.”amesema.
Getruda amewataka wakulima kutumia fursa ya mahitaji makubwa ya parachichi hiyo katika soko la kimataifa,kwani wanunuzi wa nje wamekuwa wakisifu ubora wa parachichi zinazozalishwa nchini na kuendelea kuonyesha nia ya kuzinunua kwa wingi.
Aidha amesisitiza kuwa, kuongezeka kwa uzalishaji wa parachichi aina ya Hass kutasaidia kuongeza mapato ya wakulima, kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo na kuongeza mchango wa mazao ya bustani katika uchumi wa Taifa kupitia mauzo ya nje.
