Meya wa Jiji la Arusha Maxmilian Iranghe akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Meya wa Jiji la Arusha Maxmilian Iranghe amesema kuwa Halmashauri ya Jiji imeidhinisha uwekezaji wa shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuongeza zaidi ya taa 500 za barabarani, hatua inayolenga kuimarisha usalama, kuchochea biashara za usiku na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika jiji hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Iranghe amesema Halmashauri imeendelea kutekeleza utaratibu wa kuelekeza asilimia 60 ya mapato yake ya ndani kwenye miradi ya maendeleo.
Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha husika, jiji lilikadiria kukusanya shilingi bilioni 61 za mapato ya ndani, ambapo fedha zinazobaki baada ya makato ya kisheria zinaelekezwa moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo.
Amesema mradi wa taa za barabarani utazihusisha kata mbalimbali za jiji, ukiwemo uboreshaji wa maeneo ambayo tayari yana miundombinu ya taa kama Livolosi, Kaloleni na Sekei, huku lengo likiwa kuifanya Arusha kuwa jiji linalofanya biashara saa 24 kwa kuimarisha usalama wa wananchi na wafanyabiashara.
Meya huyo amesisitiza kuwa fedha zinazotumika ni kodi za wananchi, hivyo ni wajibu wa Halmashauri kuhakikisha wananchi wanaona matokeo ya michango yao kupitia utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa jamii.
Sambamba na hilo, ameeleza kuwa jiji linaendelea kunufaika na miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara inayotekelezwa na Serikali Kuu, huku Halmashauri ikitangaza pia kuanza utekelezaji wa zabuni za miradi mipya ya barabara za ndani, mitaro ya maji ya mvua, madaraja madogo na vivuko ili kupunguza changamoto za miundombinu na mafuriko.
Katika hatua nyingine, Meya ameongeza kuwa, Halmashauri imesaini mikataba na mawakala wa ukusanyaji wa madeni na ushuru wa maegesho (parking), ambapo zaidi ya shilingi bilioni 9.2 zinatarajiwa kukusanywa kupitia mifumo hiyo.
Hata hivyo, amewataka mawakala hao kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kufuata masharti ya mikataba, akionya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wakala yeyote atakayewatoza wananchi isivyo halali.
Aidha, amewahimiza wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari kupitia mifumo ya kidijitali ikiwemo simu za mkononi na benki, akisema maboresho ya mifumo ya ukusanyaji wa mapato yameondoa ulazima wa migogoro kati ya walipakodi na mawakala.
“Halmashauri itaendelea kuwapa wananchi taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuongeza uwazi na kuwajengea imani kuwa mapato ya ndani yanatumika kuboresha huduma na miundombinu ya Jiji la Arusha.”amesema Meya
Aidha Meya ametumia fursa hiyo kuwataka mawakala kufanya kazi kwa ufanisi na weledi mkubwa na endapo wataenda kinyume mikataba yao itasitishwa.
Amesema kuwa, Halmashauri imeamua kuendelea kushirikisha na sekta binafsi katika baadhi ya shughuli za ukusanyaji wa mapato kwa kuwa hatua hiyo inachangia kuongeza ajira na kuboresha utoaji wa huduma.
Amesema mawakala waliopewa zabuni wameanza kusaini mikataba, huku mkataba wa mwisho ukisainiwa jana. Baada ya kusaini, mawakala wanatakiwa kuanza kazi mara moja kwa kufuata masharti yote yaliyowekwa kwenye mikataba yao.
Meya huyo amesisitiza kuwa Halmashauri haitasita kusitisha mkataba wa wakala yeyote atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi au atakayekiuka masharti ya mkataba.
“Mawakala wakifanya vizuri wataendelea na kazi, lakini wakishindwa kutekeleza wajibu wao au kukiuka taratibu, mkataba unaweza kusimamishwa wakati wowote,” amesema Meya .
Aidha, amebainisha kuwa utekelezaji wa mikataba hiyo utaendelea kufuatiliwa kwa karibu ili kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unafanyika kwa uwazi, ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya wananchi na Halmashauriya Jiji la Arusha.
