Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Diwani Msemo, akiongoza kikao na wawakilishi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kupitia Institute of Isotopes Co. Ltd. ya Hungary pamoja na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) cha kujadili taratibu za usafirishaji wa mabaki ya vyanzo vya mionzi vilivyotumika katika matibabu ya saratani.

Gábor Kaszás kutoka Institute of Isotopes Co. Ltd. ya nchini Hungary akichangia mada katika kikao cha majadiliano kuhusu taratibu za usafirishaji salama wa mabaki ya vyanzo vya mionzi vilivyotumika katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCi kwa ajili ya matibabu ya saratani.

Wataalamu kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) wakifuatilia kwa makini majadiliano wakati wa kikao cha kujadili  taratibu za usafirishaji salama wa mabaki ya vyanzo vya mionzi vilivyotumika katika matibabu ya saratani.

Wataalamu kutoka Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) wakishiriki katika kikao cha pamoja kilicholenga kujadili taratibu za usafirishaji salama wa mabaki ya vyanzo vya mionzi vilivyotumika katikaTaasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kwaajili ya  matibabu ya saratani. (Picha na ORCI

………….

Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), kwa kushirikiana na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), limekubaliana na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kuanza mchakato wa kusafirisha mabaki ya vyanzo vya mionzi vilivyomaliza matumizi yake katika mashine za matibabu ya mionzi kwa wagonjwa wa saratani.

Makubaliano hayo yamefikiwa leo jana katika kikao kilichowakutanisha Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo, ujumbe wa IAEA kupitia kampuni ya Institute of Isotopes Co. Ltd kutoka nchini Hungary, ukiongozwa na Mr. Gábor Kaszás, pamoja na wajumbe kutoka TAEC.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, mabaki ya vyanzo hivyo vya mionzi yatasafirishwa kwenda nchini Hungary kwa ajili ya kuhifadhiwa na kufanyiwa mchakato wa kuyahuisha kwa matumizi mengine.

Vyanzo hivyo aina ya Cobalt vilitumika katika mashine za tiba ya mionzi kwa vipindi mbalimbali kuanzia mwaka 2008, huku vingine vikitumika katika vipindi vya mwaka 2014 hadi 2020 na mwaka 2025. Baada ya nguvu ya vyanzo hivyo kupungua na kutofikia kiwango kinachohitajika kwa ajili ya matibabu, ORCI ilinunua vyanzo vipya ili kuhakikisha huduma za matibabu ya saratani zinaendelea kutolewa kwa kuzingatia viwango vya ubora.

Mchakato wa kuondoa na kusafirisha mabaki ya vyanzo vya mionzi ni utaratibu wa kawaida unaotekelezwa kwa kushirikisha mamlaka husika za ndani, TAEC na IAEA kwa kuzingatia taratibu za usalama katika usimamizi wa vyanzo vya mionzi.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mabaki ya vyanzo vya mionzi vilivyomaliza matumizi yake yanadhibitiwa na kusimamiwa kwa usalama huku vyanzo vipya vikiendelea kutumika katika kutoa huduma za matibabu ya mionzi kwa wagonjwa wa saratani.