DAR ES SALAAM

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imetakiwa kuangalia namna ya kupeleka huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo nchini Comoro kutokana na huduma hizo kutopatikana nchini humo.

Rai hiyo imetolewa leo na Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Dkt. Salim Hamad alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge kuona namna ambavyo huduma zinazotolewa na JKCI zinaweza kuwakomboa wananchi wa Comoro.

Dkt. Hamad alisema baada ya JKCI kuweka kambi maalumu ya matibabu ya moyo katika kisiwa cha Anjouan kilichopo nchini Comoro uongozi wa kisiwa hicho umeitaka JKCI kuingia mkataba nao wa kuendelea kufanya kambi za matibabu jambo ambalo linaonesha umahiri wa huduma zinazotolewa na wataalamu wa JKCI.“Nilifurahi nilipokutana na uongozi wa kisiwa cha Anjouan na kuniomba niwajulishe kuwa wanataka tuingie nao mkataba wa kufanya kambi za matibabu, hii ni hatua kubwa kwa nchi yetu katika kutoa huduma bingwa za matibabu ya moyo”, alisema Dkt. Hamad.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema uhitaji wa huduma za matibabu ya moyo nchini Comoro ni mkubwa kutokana na mwitikio uliokuwepo wakati wa kambi ya matibabu iliyofanyika mwezi Oktoba mwaka jana katika kisiwa cha Anjouan.

“Tunaandaa mkakati wa kuitangaza JKCI nchini Comoro ili tuweze kuwasaidia wananchi wa Comoro kufahamu zaidi huduma tunazozitoa na kuwapunguzia adha ya kuzifuata huduma hizi mbali na nchi ya Comoro”, alisema Dkt. Kisenge.