Na Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Mratibu wa Kampeni ya Stand for Her Land, Khadija Mrisho, amesema kampeni hiyo imefanikiwa kuwavutia wadau 38 katika ngazi ya kimataifa, kitaifa na jamii, kwa lengo la kuhakikisha wanaume na wanawake wanapata, kumiliki, kudhibiti, kunufaika, kurithi na kushiriki katika kufanya maamuzi kuhusu rasilimali ardhi.
Ameyasema hayo Agosti 12, 2026, katika Kongamano la Haki za Ardhi za Wanawake linalofanyika jijini Dodoma kuanzia Agosti 12 hadi 13, 2026, akisema kampeni hiyo ilizinduliwa mwaka 2019 ikiwa na wajumbe 25 na sasa ina takribani miaka saba ya utekelezaji.
Aidha, amesema kampeni hiyo imewafikia zaidi ya wanawake 1,500 kupitia mipango ya matumizi ya ardhi na urasimishaji wa umiliki, pamoja na kutoa msaada wa kisheria kupitia mashirika mbalimbali, ikiwemo TAWLA, WILAC, WILDAF na HakiArdhi, kwa wanawake katika mazingira na nafasi mbalimbali.
Aidha, mkakati wa kampeni hiyo unalenga kuondoa mila na desturi kandamizi zinazowazuia wanawake kumiliki na kudhibiti ardhi, kuwawezesha kiuchumi kupitia rasilimali hiyo, kuhakikisha wanashiriki katika vyombo vya maamuzi na kulinda haki zao katika maeneo yenye uwekezaji mkubwa wa ardhi.
Amesema katika kipindi cha miaka saba kampeni hiyo imeshiriki katika mapitio ya sera na sheria mbalimbali, ikiwemo Sera ya Ardhi iliyozinduliwa hivi karibuni, huku ikiendelea kushirikiana na Serikali, wizara na taasisi zake katika kutoa mapendekezo kuhusu usimamizi wa haki za ardhi za wanawake.
Ameongeza kuwa kampeni hiyo imefanikiwa kufikisha elimu ya sheria na kujenga uwezo kwa wanufaika zaidi ya laki moja, huku ikitengeneza mtandao wa takribani vinara 200 katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini wanaoendelea kutoa elimu, kutetea na kusimamia haki za ardhi za wananchi.
Kuhusu changamoto na mapendekezo, amebainisha kuwa rasilimali fedha, mila na desturi kandamizi, uelewa mdogo pamoja na sheria na sera kutokuzungumzia kwa ukubwa ulinzi wa haki za ardhi za wanawake ni changamoto zinazoendelea kuwepo, ametoa wito kwa wadau, wananchi na Serikali kuwa na nguvu ya pamoja ili kuhakikisha ajenda ya umiliki wa ardhi kwa wanawake inakuwa kubwa na sauti za wanawake zinasikika katika ngazi mbalimbali, hasa jamii.
Kwa upande wake, mwanamke kutoka Mkoa wa Rukwa, Axsa Kauzeni, amesema elimu kuhusu haki ya kumiliki ardhi aliyopata kupitia Shirika la MIICO imemsaidia kumfanya mume wake kubadili mtazamo na kumilikisha ardhi, baada ya awali kumtelekeza kwa miaka miwili pamoja na watoto kwa sababu ya suala hilo.
Kauzeni ametoa wito kwa jamii zinazoendelea kuwanyima wanawake haki ya kumiliki ardhi kuacha kufanya hivyo na kutafuta namna ya kuwawezesha wanawake kumiliki ardhi, akibainisha kuwa mwanamke akimiliki ardhi anaweza kuitumia kulima na kupata chakula cha kutunza familia.
Naye, Clara Malle kutoka Mkoa wa Manyara amesema alipitia ukatili wa kijinsia baada ya kutetea haki za mama, dada na watoto wa kike, hali iliyosababisha kufungwa jela kwa miaka minne, lakini baadaye alitoka baada ya kukata rufaa. Amesema kupitia elimu aliyopata kutoka PELUM, ameendelea kutoa elimu katika jamii na kuwa kinara wa kutetea haki.

