📍 DODOMA
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kubuni teknolojia na bidhaa zinazolenga kuongeza tija kwa wakulima na wafugaj nchini.
Dkt. Mganga ametoa pongezi hizo leo, tarehe 4 Agasti, 2026 alipotembelea banda la
VETA kwenye Maonesho ya Sikuku ya Wakulima Kitaifa (Nanenane), katika viwanja vya Dkt John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma
“tumeona jinsi VETA wanavyojitahidi kutengeneza mashine mbalimbali ambazo zinarahisisha kazi kwa wakulima na wafugaji katika maeneo yetu. Tumeona mashine
mbalimbali zinazowafaa wakulima na wafugaji kama ile ya kuchanganyia chakula cha mifugo, mashine kama hizi zinaweza kusaidia sana wananchi,”
amesema Dkt. Mganga.
Dkt Fatuma ameongeza utumiaji wa mashine rahisi kama alizoziona VETA zitasaidia kuongeza tija na faida zaidi katika uzalishaji.
“Niendelee kuwapongeza ndugu zetu wa VETA, naomba waendelee kushirikiana na wahitaji ambao ndiyo soko, ili tuweze kuendelea kusukuma etekeleazji wa Dira 2050
ninaamini kwa hizi teknolojia wametuonesha lengo la Dira tutalifikia hata kabla ya 2050 kwasababu wanachi wengi watawezeshwa kwa mitaji iliyopo na mitambo
inayotengenezwa na wabunifu kutoka veta,” ameongeza.
Katika hatua nyingine Dkt Mganga ameiomba VETA kushirikiana na ofisi za Mikoa,
Wilaya na halmashauri ili kuweza kukutanishwa na watumiaji wa bidhaa na ubunifu mbalimbali, kwani wapo vijana kupitia vikundi wanapatiwa pesa kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali ambao wanahitaji vifaa na mashine kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.
VETA inashiriki Maonesho ya Nanenane kwa lengo la kutangaza fursa za mafunzo ya ufundi stadi yanayogusa sekta za kilimo na mifugo; ubunifu waa teknolojia zinazosaidia kuongeza tija kwenye kilimo na ufugaji; ubunifu wa bidhaa zinazosaidia kupanua soko na kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya kilimo na mifugo sambamba na kaulimbiu ya maonesho hayo, _“Tambua Soko, Ongeza Tija kutekeleza Dira 2050._”



