📍DODOMA

Vijana nchini wamehimizwa kutumia nguvu kazi, maarifa na ubunifu wao kuchangamkia fursa zinazotolewa na Sekta ya Madini badala ya kusubiri misaada au mitaji kutoka serikalini, huku wakitakiwa kuanza na rasilimali walizonazo ili kujenga mafanikio ya kiuchumi.

Wito huo umetolewa kwenye Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea Kitaifa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Xinda Energy Resources Technology Import and Export Trade Co. Ltd, Abia Mafie, aliyesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupitia mafunzo, warsha na programu mbalimbali za uwezeshaji, lakini baadhi yao hushindwa kutumia maarifa hayo kwa vitendo.

“Vijana tusisubiri Serikali itupatie kila kitu. Unaweza kuanza na kidogo ulichonacho na ukakua hatua kwa hatua. Watu wengi waliofanikiwa walianza hivyo,” amesema Mafie.

Amesema Sekta ya Madini ni miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa za ajira, ujasiriamali na uwekezaji, hususan katika uchakataji na uongezaji thamani wa madini, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi wa viwanda na kuongeza mapato ya taifa.

Mafie amesema kampuni yake imewekeza katika uchakataji wa shaba na kuzalisha copper cathode yenye kiwango cha ubora cha asilimia 99.99 kinachokidhi viwango vya soko la kimataifa, hatua inayounga mkono juhudi za Serikali za kuongeza thamani ya rasilimali za madini nchini.

Ameeleza kuwa Xinda Precious Metal Resources Co. Ltd ilianza kujenga kiwanda chake mwaka 2024 na kwa sasa kina uwezo wa kuzalisha tani 50 za copper cathode kwa mwezi, huku bidhaa zake zikipata soko kutokana na ubora wake.

Kwa mujibu wa Mafie, kampuni hiyo inapanga kujenga viwanda vingine viwili vya uchakataji mkoani Dodoma ili kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za usafirishaji wa malighafi na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

Amesema uwekezaji huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku ukionesha nafasi muhimu ya sekta binafsi na ushiriki wa Watanzania katika kuongeza thamani ya madini na kuimarisha uchumi unaotegemea viwanda.