Bwana Shamba wa kampuni hiyo ,Fikiri Kalobelo  akizungumza na waandishi wa habari kuhusu teknolojia mbalimbali wanazoonesha katika maonesho hayo kwa ajili ya wakulima 
………………
Na Happy Lazaro, Arusha
WAKULIMA wametakiwa  kutembelea banda la Corteva Agriscience  katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Themi, Arusha, ili kupata elimu ya matumizi ya mbegu bora, ushauri wa kitaalamu pamoja na kujionea teknolojia mbalimbali zinazolenga kuongeza tija na uzalishaji wa mahindi nchini.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Bwana Shamba wa kampuni hiyo ,Fikiri Kalobelo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu teknolojia mbalimbali wanazoonesha katika maonesho hayo kwa ajili ya wakulima .
Fikiri amesema kampuni hiyo imeshiriki Maonesho ya Nanenane  kwa lengo la kuwaonesha wakulima teknolojia ya kisasa ya mbegu bora za mahindi aina ya Pioneer zinazofaa kwa kanda mbalimbali za uzalishaji nchini.
Fikiri ameongeza kuwa , Kampuni ya Corteva imejipanga kuhakikisha wakulima wote watakaotembelea banda lake katika Maonesho ya Nanenane wanapata huduma bora, elimu ya kitaalamu na uelewa wa kina kuhusu kilimo cha kisasa cha mahindi.
Amesema  kuwa ,wakulima watapatiwa mafunzo kuanzia uchaguzi wa mbegu bora, mbinu sahihi za uzalishaji hadi teknolojia mbalimbali zinazoweza kuongeza tija na mavuno shambani.
 “Lengo ni kuwawezesha wakulima kutumia mbinu zinazowasaidia kupata mavuno mengi na yenye ubora.”
Amesema kuwa,kwa maeneo ya ukanda wa chini, Corteva inatoa mbegu aina ya Pioneer P2848W, ambayo hukomaa ndani ya siku 80 hadi 90. Mbegu hiyo ina uwezo wa kutoa wastani wa magunia 25 hadi 30 kwa ekari endapo mkulima atazingatia kanuni bora za kilimo.
Kwa upande wa ukanda wa kati, unaopokea mvua za wastani, kampuni hiyo imeleta mbegu aina ya Pioneer P3531W na PHB 30G19, zenye uwezo wa kuzalisha wastani wa magunia 35 hadi 40 kwa ekari ambapo  amesema mbegu hizo zina punje ngumu na nzito, jambo zinazowapa wakulima faida zaidi kutokana na mfumo wa sasa wa biashara unaozingatia uzito wa mazao badala ya ujazo na zinafaa kwa kuchoma.
Aidha, ameongeza kuwa ,mbegu aina ya P3531 na PHB 30G19 zimekuwa mkombozi kwa wakulima na wafanyabiashara wengi wa mahindi mabichi nchini kutokana na ubora wake.
“Mahindi yake hudumu kwa muda mrefu baada ya kuvunwa bila kupoteza ubora, jambo linalowapa wakulima na wafanyabiashara uhakika wa soko na thamani ya mazao yao.”amesema Fikiri
Aidha, amesema kwa maeneo ya ukanda wa wa kati wenye mvua za wastani hadi mvua nyingi, amependekeza mbegu aina ya Pioneer P3812W ambayo imebuniwa kuhimili mazingira hayo.
Mbegu hiyo ina uwezo wa kutoa wastani wa magunia 35 hadi 40 kwa ekari huku ikiwa na kinga dhidi ya magonjwa ya majani na kuoza kwa mahindi kunakosababishwa na mvua nyingi.
Fikiri amefanunua kuwa, mbegu aina ya P3812W  hukomaa ndani ya siku 115 hadi 125 na huzalisha mahindi yenye ubora wa juu, hivyo kumpunguzia mkulima hasara inayoweza kusababishwa na mvua nyingi.
 Ameongeza kuwa, Corteva itaendelea kuwapatia wakulima mbegu bora pamoja na ushauri wa kitaalamu ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao nchini.
“mbali na mbegu za mahindi aina ya Pioneer, Kampuni ya Corteva pia inawapatia wakulima mbegu za Pannar zinazofaa kwa kanda zote za uzalishaji nchini.”amesema .
Ameeleza kuwa kwa ukanda wa chini na maeneo yenye mvua chache, kampuni inapendekeza mbegu aina ya PAN 3M-05, ambayo hukomaa ndani ya siku 75 hadi 80 na ina uwezo wa kuzalisha wastani wa magunia 25 hadi 30 kwa ekari ambapo amesema  mbegu hiyo ina mabua imara na hufanya vizuri si tu katika maeneo yenye mvua chache, bali pia kwenye maeneo yenye mvua za wastani.
“Kwa ukanda wa kati, Corteva inatoa mbegu aina ya PAN 53 ambayo imejipatia sifa kwa kutoa mahindi matamu yanayofaa hata kwa kuchoma ambapo mbegu hiyo ina uwezo wa kuzalisha wastani wa magunia 35 hadi 40 kwa ekari na ina bua imara linalostahimili mazingira mbalimbali ya uzalishaji.”amesema .
Fikiri  ameongeza kuwa PAN 53 ambayo imeundwa kuhimili mabadiliko ya tabia ya nchi.
Amesema mbegu hiyo hufanya vizuri katika maeneo mengi yenye mvua za wastani hadi nyingi, na hata pale mvua zinapokuwa chache bado huendelea kutoa mavuno mazuri, hivyo kuwapa wakulima uhakika wa uzalishaji licha ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Kwa ukanda wa juu, Fikiri ametaja PAN 9M-91 ambayo imepewa jina la “Jibu halisi” kutokana na ubora wake na wingi wa mavuno unaopatikana. Ni mbegu mpya yenye mavuno mengi na punje ngumu na nzito.
Aidha, amesema kampuni hiyo imeandaa mbegu za majaribio (funpacks) kwa baadhi ya wakulima, pamoja na kukusanya mawasiliano yao ili kuendelea kuwapa ushauri wa kitaalamu hata baada ya maonesho kumalizika.
Amesisitiza kuwa Corteva inaamini huduma kwa mkulima haishii kwenye kuuza mbegu pekee, bali inaendelea kwa kutoa ufuatiliaji na ushauri unaomwezesha kufikia malengo yake ya uzalishaji.
“Ndiyo maana tunasema Corteva inaboresha maisha na dhamira yetu si kuuza mbegu pekee, bali kuhakikisha mkulima anabadilika kiuchumi kupitia matumizi ya mbegu bora na teknolojia sahihi za kilimo,” amesema Fikiri.
Ameongeza kuwa utamaduni wa Corteva ni kujenga uhusiano wa karibu na wakulima kwa kuwapatia elimu na msaada wa kitaalamu wakati wote, jambo ambalo limeifanya kampuni hiyo kuwa mshirika muhimu wa wakulima katika kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha yao.