Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakari Kunenge, Julai 28, 2026, amefanya ziara ya ukaguzi wa eneo la Kongani Mpya ya Viwanda la Misugusugu, Manispaa ya Kibaha, ambapo amesema mradi huo ni hatua muhimu katika kuimarisha uchumi wa Mkoa wa Pwani na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
Mhe. Kunenge ameipongeza Manispaa ya Kibaha kwa kutenga eneo lenye ukubwa wa hekta 350 kwa ajili ya kuanzisha Kongani Mpya ya Viwanda,na kuzalisha ajira, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo aliagiza ndani ya siku 100.
Aidha kuanzisha mradi wa eneo la maegesho ya magari makubwa ya mizigo katika eneo la Misugusugu, akieleza kuwa ni mradi wa kimkakati utakaosaidia kuondoa changamoto ya magari makubwa kuegeshwa kandokando ya barabara, kuongeza usalama barabarani na kutoa huduma muhimu kwa viwanda vitakavyoanzishwa ndani ya kongani hiyo.
Mhe. Kunenge amezielekeza taasisi zote za Serikali zinazowezesha uwekezaji, ikiwemo TANROADS,TARURA, TANESCO, DAWASA na TTCL, kuhakikisha zinaimarisha na kukamilisha miundombinu muhimu katika eneo hilo kwa wakati ili kuvutia wawekezaji na kuwezesha shughuli za uzalishaji kuanza mapema.
Amesisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, halmashauri na taasisi mbalimbali ni msingi wa kufanikisha utekelezaji wa mradi huo, ambao unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya viwanda na uchumi wa Mkoa wa Pwani pamoja na Taifa kwa ujumla.
Awali, akisoma taarifa ya mradi Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, amesema eneo tayari lina huduma muhimu za maji na umeme, jambo linalolifanya kuwa kivutio kwa wawekezaji wa viwanda mbalimbali ikiwemo vya kutengeneza viatu na nguo za jinsi.
Dkt. Shemwelekwa amesema kongani hiyo, Manispaa inatarajia kuzalisha zaidi ya ajira 1,000, kuongeza mapato ya Serikali na Halmashauri pamoja na kuimarisha shughuli za uzalishaji na biashara katika Manispaa ya Kibaha.
Kwa upande wa mradi wa maegesho ya magari makubwa, amesema huduma imeanza rasmi Julai 1, 2026 na hadi sasa wastani wa magari 90 huingia na kuegeshwa kila siku katika eneo hilo.
Hatua ambayo imeanza kupunguza kero ya madereva kuegesha magari katika maeneo yasiyo rasmi na kuongeza utaratibu katika sekta ya usafirishaji.
Kwa wananchi wa Kibaha, utekelezaji wa kongani hiyo mpya ya viwanda unaashiria matumaini mapya ya ajira, ongezeko la shughuli za biashara na kuimarika kwa huduma za kijamii, huku ukiiweka Manispaa ya Kibaha katika nafasi muhimu ya kuwa kitovu cha maendeleo ya viwanda Mkoa wa Pwani.

