Mwenyekiti wa mashindano hayo ya Redcross Marathon Arusha  2026,Dora Mushi akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo 
Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Fahari Travel Agents ,Mariam Haji ambao ni miongoni mwa wadhamini akizungumza katika kikao hicho na waandishi wa habari leo
Mtawala kutoka ADN Care ,Shazmeen Abas akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo  
…………
Na Happy Lazaro, Arusha
ZAIDI  ya watu 500  wanatarajiwa kushiriki kwenye mashindano ya Redcross Marathon itakayofanyika agosti 2,2026 katika.uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha .
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha Mwenyekiti wa mashindano hayo ya Redcross Marathon Arusha  2026,Dora Mushi amesema kuwa,maandalizi yote yameshakamilika na kuwa mbio hizo zitafanyika  katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
“kutakuwepo na.mbio za kilometa 21,10,5  na kilometa 2.5 kwa ajili ya watoto  na washindi watapewa kiasi cha fedha taslimu pamoja na medali.”amesema Dora.
Amesema marathon hiyo inalenga kuwakutanisha wananchi katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kuhamasisha afya bora, vipimo vya afya na uchangiaji wa kusaidia makundi yenye uhitaji katika jamii.
“Tunawakaribisha ndugu zetu wote agosti  2 mwaka huu,katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid kwani kutakuwa na mambo mengi mazuri ikiwemo mkesha uwanjani, mazoezi, upimaji wa damu na uchunguzi wa afya,” amesema.
Ameongeza kuwa ,wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi na kuwaalika ndugu, marafiki na majirani zao ili kushiriki katika marathon hiyo ambayo imeandaliwa kwa lengo la kuleta mshikamano na kusaidia jamii.
Dora amesema kuwa mashindano hayo ya  Red Cross Marathon  Arusha  imekusudia kuwafikia watu wenye mahitaji maalum, wakiwemo watoto yatima, watu wenye ulemavu, wazee pamoja na vijana walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya wanaopatiwa huduma katika vituo vya urekebishaji tabia.
“Lengo letu kubwa ni kufikia jamii ambayo ni wahitaji kwa kuna watoto yatima, walemavu, wazee na vijana wetu ambao wameathirika na dawa za kulevya ambao wanahitaji msaada ambapo sehemu ya mapato yanayopatikana kupitia marathon hiyo yatatumika kuwasaidia watu waliokumbwa na majanga mbalimbali wakiwemo watoto ,watu wenye ulemavu na makundi mengine yenye.uhitaji ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza mateso ya wananchi.”amesema Dora
Amewataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi na kushirikiana na Tanzania Red Cross kuhakikisha marathon hiyo inakuwa na mafanikio makubwa katika kusaidia jamii na kuimarisha afya za wananchi.
Kwa upande wake Mhamasishaji   Mkuu wa Redcross Tanzania ,Dokta Christopher Nzella amesema kuwa ,kaulimbiu ya marathon ya Run for Health, Run for Humanity” inaendana na dhamira yake ya kutoa huduma za afya na misaada ya kibinadamu kwa wananchi, huku likisisitiza kuwa afya ni moja ya maeneo ya msingi katika shughuli zake.
Amesema kuwa ,Tanzania Redcross  hutoa huduma mbalimbali za afya, zikiwemo afya ya jamii, afya ya mama na mtoto pamoja na huduma kwa wakimbizi ambapo pia hushirikiana kwa karibu na Serikali kutoa msaada kila kunapotokea majanga au milipuko ya magonjwa kama Ebola na UVIKO-19.
Amesema kaulimbiu hiyo pia inaakisi kanuni za msingi za Msalaba Mwekundu, hususan ubinadamu na kujitolea, akibainisha kuwa maelfu ya watu wanaojitolea ndiyo nguvu kubwa inayowezesha shirika hilo kuwafikia wananchi wanaohitaji msaada katika nyakati za dharura.
Kwa.upande wake , Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Fahari Travel Agents ,Mariam Haji amesema kuwa wamekiwa.wadhamini kwenye mbio hizo kwani wamekuwa wakihamasisha swala zima la kufanya mazoezi kwa afya hivyo kupitia mbio hizo ni  wajibu wa kila kujitokeza kwa lengo la kushiriki.
“Tunawashukuru sana Redcross Arusha kwa kuona umuhimu wetu na kuweza kutuchagua kuwa wafadhili na sisi tunawaahidi kuendelea kuwa bega kwa bega katika kushirikiana katika kila hatua kwani mazoezi ni afya na ni muhimu sana kwa kila binadamu “amesema Mariam 
Naye Mtawala kutoka ADN Care ,Shazmeen Abas amesema kuwa ,wamekuwa wakitoa huduma  za matibabu kwa watu mbalimbali ambapo swala la kufanya mazoezi wamekuwa wakilipa kipaumbele sana ndo maana wameweza kuwa wafadhili wa mbio hizo.
Aidha ametoa wito kwa wananchi mbalimbali kujitokeza kwa wingi katika mbio hizo kwani mazoezi ni afya na kila mmoja ana wajibu wa kufanya mazoezi kwa lengo la kuimarisha afya ya mwili.
Aidha amewataka wananchi kuendelea kushiriki shughuli kama hizo kwa kuwa zinachangia kuboresha huduma za afya na kuokoa maisha ya Watanzania.