Katika kuendeleza dhamira yake ya kuchangia maendeleo ya jamii kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSI) chini ya kampeni yake ya #PSSSFKaribuNaJamii, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umekabidhi rasmi mradi wa miundombinu wenye thamani ya Shilingi milioni 25 katika Shule ya Msingi Majani Mapana iliyopo mkoani Tanga.Mradi huo unahusisha ujenzi wa chumba cha darasa, chumba cha mapumziko pamoja na vifaa mbalimbali vya michezo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Bw. Kwame Temu alieleza kuwa msaada huo unalenga kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata haki yao ya msingi ya elimu. Alisisitiza kuwa hatua hiyo itawasaidia wanafunzi hao kujifunza katika mazingira yanayowawezesha kujifunza kwa ufanisi, kushiriki katika michezo na kukuza vipaji vyao mbalimbali.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Kata ya Nguvumali, Bi. Lilian Shetui, aliishukuru PSSSF kwa mchango huo akieleza kuwa miundombinu hiyo itaongeza ubora wa huduma za elimu shuleni hapo. Kwa niaba ya Afisa Elimu Shule za Awali na Msingi wa mkoa huo, Bi. Lilian alipongeza PSSSF kwa kuona umuhimu wa kundi hilo na kutoa msaada utakaokuwa na tija kubwa kwa watoto hao.


