NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Viti Maalum Vijana Taifa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jasmin Ng’umbi, amekutana na viongozi wa makundi mbalimbali ya vijana mkoani Iringa na kusikiliza changamoto zinazowakabili, huku akiahidi kuzifikisha katika mamlaka husika na kuzitafutia ufumbuzi.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi za CCM Mkoa wa Iringa kiliwakutanisha viongozi wa bodaboda, bajaji, machinga, jogging clubs, wasanii wa filamu na makundi mengine ya vijana kwa lengo la kujadili masuala ya maendeleo na ustawi wa vijana.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho, Ng’umbi alisema amefurahishwa na ushirikiano mkubwa alioupata kutoka kwa viongozi wa makundi hayo na kusisitiza kuwa maoni na changamoto zote zilizowasilishwa zimepokelewa na zitafanyiwa kazi kwa kadri ya uwezo wake kama mwakilishi wa vijana bungeni.
Alisema mbali na kupokea changamoto hizo, kikao hicho kilitoa fursa ya kuelimishana kuhusu wajibu wa vijana katika kujiletea maendeleo, kulinda amani, kuimarisha umoja na kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo yao.
Ng’umbi aliwataka vijana wa Iringa kuendelea kuwa wamoja bila kujali tofauti za makundi au kazi wanazofanya, akieleza kuwa mshikamano ni msingi muhimu wa maendeleo na utatuzi wa changamoto zinazowakabili.
Akizungumzia suala la ajira, alisema ni changamoto inayozikabili si vijana wa Iringa pekee bali Tanzania nzima, hivyo kuna umuhimu wa kutumia mbinu mbalimbali za kupunguza tatizo hilo badala ya kutegemea ajira rasmi pekee.
Alisema serikali kupitia halmashauri inaendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, huku pia akisisitiza vijana kutumia fursa za mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali pamoja na kujitokeza kufanya kazi yoyote halali itakayowaingizia kipato.
“Tumekubaliana sisi kama vijana wa Iringa tusichague kazi. Kazi yoyote halali inayoweza kutuinua kiuchumi inapaswa kufanywa kwa bidii,” alisema Ng’umbi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Bajaji Mkoa wa Iringa, Merab Titus Kihwele, alimpongeza mbunge huyo kwa kuonyesha utayari wa kukutana na makundi ya vijana na kusikiliza changamoto zao.
Alisema miongoni mwa masuala yaliyowasilishwa ni changamoto za upatikanaji wa leseni, mahitaji ya kuwawezesha vijana kiuchumi pamoja na pendekezo la kuanzishwa ligi itakayoshirikisha makundi mbalimbali ya vijana kama bodaboda, bajaji na machinga ili kuimarisha mshikamano.
“Ni mara ya kwanza kuona mbunge wa vijana akiita makundi haya kwa pamoja, akayasikiliza na kuahidi kuyawakilisha mbele ya serikali. tunampongeza kwa hatua hii,” alisema Kihwele.
Naye Katibu wa Tanzania Drama and Film Actors Association (TDFAA) Mkoa wa Iringa, Hassan Rafiq, alisema chama hicho kimefurahishwa na mwaliko wa kushiriki kikao hicho, akibainisha kuwa kinaonesha dhamira ya Mbunge Jasmin Ng’umbi ya kuyaunganisha makundi yote ya vijana na kushirikiana nayo katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Rafiq alisema ushirikiano kati ya viongozi na makundi ya vijana ni muhimu katika kujenga mazingira yatakayowawezesha vijana kujikwamua kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
