NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, ametoa wito kwa wananchi, wadau wa michezo, wafanyabiashara na wazawa wa Iringa waliopo ndani na nje ya mkoa kushirikiana kuanzisha mfuko maalumu utakaowezesha kurejeshwa kwa timu ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoiwakilisha Iringa.
Ngajilo alitoa kauli hiyo wakati wa kukabidhi vifaa vya michezo kwa timu 16 zilizofuzu hatua ya 16 bora ya mashindano ya Ngajilo Super League 2026 yaliyofanyika katika Uwanja wa Samora mjini Iringa.
Alisema baada ya miaka 15 tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 2010, sasa umefika wakati wa kuyatumia kama msingi wa kuimarisha maendeleo ya soka na kufanikisha ndoto ya mkoa kuwa na timu ya Ligi Kuu.
“Majadiliano ya kuwa na timu ya Ligi Kuu yamekuwa mengi sasa umefika wakati wa kugeuza maneno kuwa vitendo kwani Iringa inahitaji timu itakayobeba heshima na kuitangaza mkoa wetu nchini,” alisema Ngajilo.
Alisisitiza kuwa timu hiyo haitakuwa mali ya wilaya au jimbo moja bali ya Mkoa mzima wa Iringa, akiwataka wananchi wa Kilolo, Mufindi, Isimani, Kalenga, Iringa Mjini pamoja na wazawa wanaoishi Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Njombe, Morogoro na maeneo mengine kushiriki katika ujenzi wa timu hiyo.
Ngajilo alisema changamoto kubwa si kununua timu bali ni kuimudu kifedha, hivyo akashauri kuanzishwa mfumo wa kisasa wa usajili wa wanachama na uchangiaji wa fedha kwa njia za kidijitali ili kuhakikisha timu inakuwa na chanzo cha mapato cha uhakika.
Alieleza kuwa hata michango midogo ya shilingi 1,000 kwa mwezi kutoka kwa maelfu ya wananchi inaweza kuwa msingi wa kuiendesha timu kwa ufanisi, huku akipendekeza kuundwa kwa kamati maalumu ya fedha itakayosimamia ukusanyaji na matumizi ya michango hiyo.
Ngajilo aliwataka viongozi wa soka kuanza kujenga mifumo imara ya kifedha kabla ya kuanza mchakato wa kununua timu, akisema ni muhimu kuhakikisha kuna fedha za kutosha kwa ajili ya mishahara ya wachezaji, safari, malazi, vifaa na mahitaji mengine ya uendeshaji.
Aidha aliwahimiza wadau wengine kujitokeza kuunga mkono Ngajilo Super League ili maendeleo ya soka yasitegemee mfadhili mmoja pekee, huku akiwapongeza viongozi wa Chama cha Soka Wilaya ya Iringa (IDFA) kwa usimamizi mzuri wa mashindano hayo.
Katibu wa IDFA, Yahaya Mpelembwa, alimpongeza Mbunge Ngajilo kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya soka kwa miaka mingi na kusema mchango wake umeiwezesha ligi hiyo kukua kutoka ngazi ya Manispaa hadi kushirikisha timu kutoka majimbo ya Iringa Mjini, Isimani na Kalenga.
Alisema timu 16 zilizofuzu zimepatikana baada ya ushindani mkali wa ligi na sasa zitacheza hatua ya mtoano (knockout) hadi kupatikana bingwa atakayewakilisha Wilaya ya Iringa katika mashindano ya ngazi ya mkoa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa IDFA, Joel Musiba, alisema Ngajilo ameendelea kuwa mdhamini mkuu wa ligi hiyo kwa misimu zaidi ya mitano bila ubaguzi, jambo lililochochea ukuaji wa soka la wilaya.
Musiba alisema chama hicho hakifanyi siasa bali kina wajibu wa kushirikiana na wadau wote wanaosaidia maendeleo ya michezo, akiwataka viongozi wa timu kuhakikisha wanathamini wadhamini kwa kuvaa jezi zenye nembo ya mdhamini rasmi wa mashindano.
Pia alimuomba Mbunge huyo kuendelea kuisaidia timu itakayotwaa ubingwa wa Ngajilo Super League katika safari yake ya kushiriki mashindano ya ngazi ya mkoa ili kuongeza nafasi ya Iringa kupata timu itakayopanda madaraja hadi kufikia Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mashindano ya Ngajilo Super League yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya soka na kuimarisha ushindani wa timu za wilaya, huku wadau wakiamini kuwa yanaweza kuwa nguzo ya kurejesha hadhi ya soka la Mkoa wa Iringa

