NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Nancy Nyalusi, amesema ujenzi wa jengo jipya la Mama na Mtoto ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya na unatarajiwa kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga huku ukiimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa.
Nyalusi alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa jengo hilo uliohudhuriwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ambapo alimkaribisha wilayani Iringa na kueleza kuwa wananchi wa mkoa huo wanaendelea kushuhudia matokeo makubwa ya uwekezaji wa Serikali katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Alisema Serikali imeendelea kuonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha sekta ya afya kwa kujenga miundombinu ya kisasa inayowezesha wananchi kupata huduma bora karibu na maeneo yao.
“Jengo hili la Mama na Mtoto litasaidia kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga, huku likiboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya hivyo tunamshukuru sana Rais na Serikali kwa kuendelea kutuletea miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi,” alisema Nyalusi.
Nyalusi alisema kuwa uwekezaji unaofanywa katika sekta ya afya umeongeza matumaini kwa wananchi, hasa wanawake na watoto ambao ndio wanufaika wakuu wa huduma hizo.
Pia aliwataka wananchi kutunza miundombinu hiyo ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi kwa miaka mingi ijayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alisema ujio wa Waziri wa Ujenzi ni fursa kwa Serikali kujionea hatua kubwa ambazo Mkoa wa Iringa umezipiga katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisema uwepo wa Waziri huyo ni ishara ya namna Serikali ya Rais inavyofuatilia kwa karibu maendeleo ya miradi ya umma na kuhakikisha uwekezaji unaofanywa unaleta matokeo yaliyokusudiwa.
“Leo tumepata nafasi ya jicho la Mheshimiwa Rais kupitia Waziri wa Ujenzi mh Ulega kuona ni kwa kiwango gani tumepiga hatua kama wana Iringa,” alisema Kheri.
James aliipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa maandalizi mazuri ya hafla hiyo, akisema yameonyesha uwezo wa mkoa katika kupokea wageni wa kitaifa na kusimamia shughuli za maendeleo.
Aidha, aliisifu Hospitali ya Manispaa ya Iringa kwa ubora wa huduma zinazotolewa na watumishi wake, akieleza kuwa hospitali hiyo imekuwa mfano wa utoaji wa huduma zenye utu na kuwapa wagonjwa faraja tangu wanapowasili.
“Hii ni miongoni mwa hospitali zenye watumishi bora sana. Hapa tuna wahudumu wazuri ambao hata kabla hawajakupa dawa, maneno yao yanawafariji wagonjwa. Kuanzia mapokezi namna wananchi wanavyopokelewa, jambo hilo linatia moyo sana,” alisema.
Kheri alisema mafanikio ya sekta ya afya hayategemei ujenzi wa majengo pekee bali pia yanahitaji watumishi wenye weledi, maadili na moyo wa kuwahudumia wananchi kwa upendo
Uzinduzi wa ujenzi wa jengo hilo la Mama na Mtoto unatajwa kuwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuendelea kuboresha huduma za afya nchini kwa kujenga miundombinu ya kisasa,
 kuongeza ubora wa huduma na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika kwa akina mama na watoto wachanga, huku wananchi wa Mkoa wa Iringa wakieleza matumaini makubwa kuwa huduma zitaboreshwa zaidi baada ya kuanza kutumika kwa jengo hilo.