Wafugaji na Wafanyabiashara wa Mifugo Katika Kijiji na Kata ya Mwimbi, Wilaya ya Kalembo Mkoani Rukwa wametakiwa kuungana na kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi ambavyo vitasaidia kulinda mifugo, pamoja na kuwafichua wezi wa Mifugo Kijijini hapo.

Akizungumza na Kusikiliza kero za Wafugaji na Wafanyabiashara hao wa Mifugo, leo Julai 24 2026, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini (STPU) Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Simon Pasua, amesema kuwa wezi wa Mifugo wanatoka katika maeneo yao hivyo ni jukumu lao kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi ambavyo vitasaidia kulinda mifugo hiyo, huku akikemea tabia ya kuwaficha wezi wa mifugo baina yao.

SACP Pasua amesema kuwa Jeshi la Polisi litawasilisha katika mamlaka husika kero zote zilizoainishwa katika kikao hicho ikiwemo kuwekwa uzio katika eneo la mnada pamoja na uboreshwaji wa miundombinu muhimu, hatimaye kuboresha sekta ya biashara ya mifugo Nchini kwa manufaa yao na Taifa kwa Ujumla.

Sambamba na hayo Kamanda huyo pia amewataka wasimamizi wa mnada huo kuhakikisha kila anayenunua mifugo anakatia ushuru na kupewa risiti, huku akimuagiza Mkaguzi Kata kuimarisha doria katika maeneo ya mipakani ili kuzuia utoroshwaji wa mifugo nje ya Nchi.

Naye Afisa Mifugo wa Kata hiyo, Conrad Ndungulu amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kufika na kutoa elimu katika mnada huo, huku akisema kuwa atahakikisha maelekezo yote yanasimamiwa ipasavyo, ikiwemo kutoa risiti kwa wanunuzi wa Mifugo pamoja na kuhakikisha hakuna mfugaji anayelipa ushuru mara mbili kama ambavyo walieleza awali katika kero zao.