Kagera.
Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, amefanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Lusahunga–Benako–Rusumo yenye urefu wa kilomita 92, akieleza kuwa ni moja ya barabara za kimkakati zinazochochea uchumi wa nchi kutokana na kutumiwa na malori makubwa yanayoingia na kutoka nchini kupitia mpaka wa Rusumo
Katika ziara hiyo, Waziri Ulega amewataka wananchi kuwa walinzi na watunzaji wa miundombinu ya barabara ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Wananchi wa maeneo yanayopitiwa na mradi huo wameiomba Serikali kuhakikisha kunajengwa njia za watembea kwa miguu wakati wa ujenzi unaendelea, kufungwa taa za barabarani ili kuwezesha shughuli za biashara nyakati za usiku, pamoja na kujengwa stendi maalumu ya maegesho ya malori katika eneo la Rusahunga.
Akijibu ombi hilo, Waziri Ulega amesema Serikali ya Kijiji cha Rusahunga tayari imetoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa maegesho hayo, na kumuagiza Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na wataalamu kutoka TANROADS kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa mradi huo kwa haraka.
Amesema maegesho hayo yataongeza mapato ya Halmashauri na kutoa fursa zaidi za biashara kwa wananchi wa eneo hilo.
Aidha, Waziri Ulega amewataka wananchi kupuuza hoja zinazobeza juhudi za Serikali kuhusu ongezeko la deni la taifa, akieleza kuwa fedha zinazokopwa zinaelekezwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu muhimu inayowanufaisha wananchi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa mkandarasi, kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), Mhandisi Hamza Feisal, amesema mradi huo ulianza Julai mwaka 2023 na unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 42 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 209.
Amesema hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 73.97, huku kata nne zinazopitiwa na mradi huo zikinufaika na utekelezaji wa miradi ya kijamii ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na miradi ya elimu kama sehemu ya kurudisha kwa jamii (Corporate Social Responsibility – CSR). Ameongeza kuwa ujenzi unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika kwa wakati.
Naye Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera, Mhandisi Julius Festo, amesema utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri kutokana na ushirikiano mzuri kati ya TANROADS na mkandarasi. Amesema hadi sasa mradi umefikia mwezi wa 37 kati ya miezi 42 iliyopangwa, huku ujenzi wa makalavati ukikamilika kwa asilimia 100.
Amefafanua kuwa mkandarasi tayari amelipwa malipo ya awali ya zaidi ya shilingi milioni 25, sawa na asilimia 15 ya malipo ya awali, na kwa ujumla Serikali tayari imelipa zaidi ya shilingi bilioni 91 kwa mkandarasi, huku mkandarasi mshauri akilipwa zaidi ya shilingi bilioni 3.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Ngara, Mheshimiwa Dotto Bahemu, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuitekeleza miradi mikubwa ya maendeleo wilayani Ngara, akisema ujenzi wa barabara hiyo utarahisisha usafirishaji, kuchochea biashara na kuboresha maisha ya wananchi.

