NA: DK. REUBENI LUMBAGALA
Maji safi na salama ni hitaji muhimu la wananchi waishio mijini na vijijini. Serikali inalo jukumu la kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma hiyo ili kuwezesha kufanyika kwa shughuli za kijamii na kiuchumi kwa ufanisi na ubora.
Kutokana na uhitaji mkubwa wa raslimalifedha za kugharamia miradi ya maji, serikali inasisitiza ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi (PPP).
Hilo linafanyika kwa nia njema ya kuharakisha usambazaji wa maji kwa wananchi. Watu binafsi, taasisi za dini, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa maendeleo, wanakaribishwa kuongeza nguvu ya usambazaji maji kwa wananchi.
Aidha, wadau hao wanaweza kusaidia uchimbaji wa visima, kuanzisha miradi midogo na mikubwa ya maji, ili wananchi waweze kupata huduma hiyo kwa kuzingatia ukweli kuwa “Maji ni Uhai”.
Kimsingi, serikali imekuwa ikipata ushirikiano mzuri kutoka sekta binafsi katika kugharamia miradi ya maji. Katika malengo na mikakati ya Wizara ya Maji katika bajeti ya mwaka 2026/2027, ni pamoja na kuhimiza ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi katika kugharamia miradi ya maji.
Hakika, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga Uwasa) imekuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa kuishirikisha sekta binafsi kikamilifu katika kuongeza nguvu ya usambazaji maji kwa wananchi.
Ni hivi: Kupitia ubunifu wa kutafuta fedha mbadala (alternative financing), Tanga Uwasa kupitia Hatifungani ya Kijani, imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 53.12 kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali.
Fedha hizo zinatumika kuongeza mtandao wa usambazaji maji kwa wananchi waishio Jiji la Tanga na wilaya za Mkinga, Muheza na Pangani, huku wakitarajia kurejesha fedha hizo pamoja na gawio kwa wawekezaji wake.
Ubunifu huu unatokana na changamoto za kibajeti, ambapo kusubiri fedha kutoka serikali kuu pekee ni kuchelewesha maendeleo kwa wananchi kwani maji ni kiungo muhimu wa kuwezesha shughuli nyingi za kijamii na kiuchumi.
Hivyo basi, ipo haja ya mamlaka nyingine za maji, kuiga ubunifu huu wa Tanga Uwasa wa kutafuta fedha mbadala za kuwezesha usambazaji wa maji safi, salama na yenye kutosheleza kwa wananchi.
Mei 16, 2024, Tanga Uwasa iliorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kupitia ubunifu wake wa hatifungani ya miundombinu ya maji na utunzaji wa mazingira.
Katika hafla hiyo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema “Upatikanaji wa fedha kupitia Hatifungani kama hii ya Tanga, inasaidia juhudi za serikali na kuharakisha utoaji wa huduma bora ya maji kwa wananchi. Natoa rai kwa mamlaka nyingine za maji, kijifunza kupitia hatifungani ya Tanga Uwasa na kuiga mfano huu”.
Hivi karibuni, Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Nadir Abdullatif, alitembelea mradi mkubwa wa maji unaofadhiliwa kwa fedha za Hatifungani ya Kijani ya Tanga Uwasa, kujifunza namna mamlaka hiyo ilivyofanikiwa kutumia fedha mbadala kugharamia miradi ya maji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Uwasa, Mhandisi Geoffrey Hilly, amesema mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maji yamechangiwa na ushiriki wa sekta binafsi, hivyo serikali itaendelea kushirikiana nao bega kwa bega ili kufanikisha dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kumtua ndoo mama kichwani na kuongeza kasi ya maendeleo kupitia sekta ya maji.

Maoni: 0620 800 462.
