Mkongwe wa tasnia ya habari nchini, Bi. Rose Haji Mwalimu, amesema mfumo wa ithibati ya waandishi wa habari umeleta mabadiliko makubwa kwa kurejesha heshima ya taaluma hiyo na kusaidia kuwatofautisha waandishi wenye weledi na watu wasiokuwa na sifa za kitaaluma.Bi. Rose amesema hayo leo, tarehe 23 Julai, 2026, mara baada ya kupokea kitambulisho chake cha Uandishi wa Habari katika Ofisi za Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), jijini Dar es Salaam baada ya kukidhi vigezo kwa Mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari. 

Amesema kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo, tasnia ya habari ilikuwa imekumbwa na changamoto ya watu wasiokuwa na taaluma kujihusisha na shughuli za uandishi wa habari, hali iliyochafua taswira ya waandishi wote.

“Tasnia ilikuwa imevamiwa na makanjanja kwa sababu wote tulikuwa tumewekwa kwenye kapu moja la samaki. Ukiukwaji unaoonekana kwenye mitandao ya kijamii ulionekana kana kwamba unatokana na waandishi wote, wakati uandishi wa habari ni taaluma inayoheshimika,” amesema Bi. Mwalimu.

Ameongeza kuwa kitambulisho cha ithibati ni alama ya heshima na utambulisho wa kitaaluma kwa waandishi wa habari na watangazaji, kwani kinawasaidia wananchi na wadau kuwatambua waandishi halali.

“Kitambulisho hiki kinaheshimisha uandishi wa habari na utangazaji. Kwa sasa kuna watu wengi wanaopotosha kupitia mitandao ya kijamii, hivyo mfumo huu unatofautisha makanjanja na waandishi wenye taaluma,” amesema Bi. Mwalimu.

Bi. Rose Haji Mwalimu ni miongoni mwa wakongwe wa tasnia ya habari nchini, akiwa amewahi kufanya kazi Radio One na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). Kupokea kwake ithibati ni sehemu ya utekelezaji wa mfumo unaolenga kuimarisha weledi, uwajibikaji na maadili katika taaluma ya uandishi wa habari nchini.