Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda, amezitaka timu zote za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuweka mikakati endelevu ya kutambua na kuendeleza vipaji vya vijana wenye uwezo wa michezo ili kujiunga na jeshi, hatua itakayohakikisha kunakuwa na mwendelezo wa wanamichezo wenye uwezo mkubwa pindi wengine wanapostaafu au kumaliza muda wao wa kushiriki mashindano.
Jenerali Mkunda ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati wa kilele cha Mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF CUP 2026), ambapo amesema mashindano hayo yanapaswa kutumika kama jukwaa la kuibua vipaji vitakavyoliwezesha JWTZ kuendelea kuwa na wanamichezo bora kwa miaka ijayo.
Aidha, amesisitiza kuwa pamoja na kukuza michezo, jukumu kuu la JWTZ linaendelea kuwa kulinda amani na mipaka ya Taifa ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama na yenye utulivu. Amesema michezo ni nyenzo muhimu ya kujenga afya, mshikamano na utayari wa wanajeshi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Katika fainali ya mashindano hayo, timu ya JKT ilitwaa ubingwa baada ya kuichapa DFHQ mabao 3-1 mbele ya viongozi mbalimbali wa jeshi na wadau wa michezo. Jenerali Mkunda pia amewaasa wanamichezo hao kuendelea kujitunza, kuzingatia nidhamu na sheria za michezo pamoja na kujiweka katika kiwango bora cha utimamu wa mwili wanaposhiriki mashindano ya ndani na ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya CDF CUP 2026, Brigedia Jenerali Saidi Hamis Saidi, amesema mashindano hayo yamefikia malengo yaliyokusudiwa kutokana na ushiriki mkubwa wa vikosi mbalimbali na kufanikiwa kuibua vipaji vipya. Amesema CDF CUP imeendelea kuwa chachu ya kuimarisha mshikamano, ushirikiano na kubadilishana uzoefu miongoni mwa wanajeshi, huku ikitoa fursa ya kupata wanamichezo bora watakaoiwakilisha JWTZ katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.

