Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akisalimiana na Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Melckzedek Mbise, baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa N’Djamena nchini TChad, kwa ajili ya kushiriki kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), Jukwaa la Maji barani Afrika, (African Water Forum; from vision to action), linalotarajiwa kufanyika nchini humo.

Naibu Waziri wa Fedha, Tanzania, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), (katikati), Naibu Waziri wa Maji, Tanzania, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb), (kushoto), wakimsikiliza Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Melckzedek Mbise, wakati akitoa maelezo mafupi baada ya kuwapokea katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa N’Djamena nchini TChad, kwa ajili ya kushiriki kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), Jukwaa la Maji barani Afrika, (African Water Forum; from vision to action), linalotarajiwa kufanyika nchini humo. Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Melckzedek Mbise, akijadiliana jambo na Afisa Utumishi, Wizara ya Fedha, Tanzania, Bi. Limy Kahabi, mara baada ya kumpokea, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), (hayupo pichani), alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa N’Djamena nchini TChad, kwa ajili ya kushiriki kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), Jukwaa la Maji barani Afrika (African Water Forum; from vision to action), linalotarajiwa kufanyika nchini humo.

Na. Asia Singano, WF, N’Djamena TChad

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), amewasili jijini N’Djamena, nchini Chad, kushiriki Jukwaa la Maji Barani Afrika kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb).

Jukwaa hilo la ngazi ya juu, lenye kaulimbiu “African Water Forum: From Vision to Action”, linatarajiwa kuwakutanisha Wakuu wa Nchi za Afrika, Mawaziri wa Fedha na Maji, pamoja na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali kujadili namna ya kuimarisha usalama wa maji, kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo na kujenga ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano huo ambao utaongozwa na Rais wa Jamhuri ya TChad, Mhe. Mahamat Idriss Deby, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB), una lengo la kuharakisha upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na kuboresha mifumo ya usafi wa mazingira katika nchi za Afrika.

Vilevile, masuala yatakayojadiliwa ni pamoja na kuongeza uwekezaji katika sekta ya maji na umwagiliaji, kuimarisha usimamizi wa mabonde ya mito inayoshirikishwa na nchi mbalimbali, kuboresha ushirikiano wa kikanda, pamoja na kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika kugharamia miradi ya maendeleo ya maji.

Washiriki watajadili mikakati ya kuongeza rasilimali fedha kwa ajili ya sekta ya maji, kuandaa mipango ya kitaifa ya uwekezaji katika sekta hiyo (National Water Compacts), na kutafuta suluhisho la kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wa Tanzania, ushiriki katika jukwaa hilo unatarajiwa kuimarisha ushirikiano na washirika wa maendeleo, taasisi za fedha pamoja na wawekezaji binafsi, huku ukitoa fursa ya kuitangaza nchi kama eneo lenye mazingira mazuri ya uwekezaji katika miundombinu ya maji.

Aidha, Tanzania itanufaika kwa kujifunza mbinu mbalimbali za ubunifu katika kugharamia miradi ya maendeleo, ikiwemo matumizi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi katika kipindi cha ufinyu wa rasilimali za Serikali.

Mkutano huo pia unatarajiwa kuchangia jitihada za Tanzania katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hadi asilimia 70.

Katika safari hiyo, Mhe. Luswetula ameambatana na Naibu Waziri wa Maji, Tanzania, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb), Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Melckzedek Mbise, pamoja na maafisa wengine wa Wizara ya Fedha.