…………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Wafanyabiashara Halmashauri ya jiji la Dodoma watakiwa kutunza mazingira wanayofanyia biashara ili kuweza kulinda afya zao na wateja wao.
Kauli hiyo ilitolewa na Ofisa Masoko wa Jiji hilo, James Yuna, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu suala la utupaji wa takataka zinazotokana na bidhaa za matunda zinazoletwa na wafanyabiashara wa nje ya jiji.
Yuna amesema wafanya biashara wanaonasababisha kusambaza kwa taka za vifungashio vya matunda sokoni uongozi wa halmashauri utawachukulia hatua za kisheria.
“Kwasasa Jiji hilI litaanza kutoza faini kwa magari yote na wale watakaobainika kutupa vifungashio hivyo kwenye madampo yasiyo rasmi ya kutupa taka hizo”,amesema Yuna.
Yuna amesema kuwa vifungashio hivyo havipaswi kuachwa na kutupwa kwenye madampo yaliyopo kwenye masoko bali taka hizo zinatakiwa kupelekwa dampo lililotengwa Chidaya Ntyuka.
Yuna ameongezea kuwa hivi sasa kuna baadhi ya wafanyabiashara wanaoleta bidhaa za matunda zikiwa zimefungashwa na majani na wakishusha huku wakiacha sokoni.
Akibainisha amesema kuwa wanaofanya kitendo hicho wanakiuka kanuni na sheria.
“Halmashauri imeshatoa katazo juu ya vifungashio hivyo vinavyoletwa kwenye masoko yake na tumewataka wafanyabiashara wote wanaoleta na kushusha bidhaa zao zikiwa kwenye vifungashio baada ya kumaliza wanatakiwa kuondoka navyo na kupeleka dampo la Chidaya kulikopangwa kutupa takataka zote,”ameeleza.
Hata hivyo amesema baadhi ya masoko ya jiji hilo imebainika kuwa madampo yake wafanyabiashara wanakiuka kanuni za usafi kwa kutupa vifungashio hivyo vilivyopigwa marufuku na Halmashauri.