Kiwanda kikubwa cha kuchakata madini ya kinywe (Graphite) kinachomilikiwa na Kampuni ya Permanent Mineral kilichopo Kijiji cha Kandasikira, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, kimezinduliwa rasmi na Mwenge wa Uhuru 2026, huku kikitajwa kuwa hatua muhimu katika kukuza uchumi wa viwanda, kuongeza ajira na mapato ya Serikali kupitia kodi.
Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 50 unatarajiwa kutoa ajira kwa Watanzania wengi, hususan wananchi wa eneo la Simanjiro, sambamba na kuongeza thamani ya madini yanayozalishwa nchini badala ya kuuzwa yakiwa ghafi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, alisema uwekezaji huo unaonesha kuwa Tanzania inaendelea kuwa kivutio cha wawekezaji wa kimataifa kutokana na mazingira mazuri ya biashara, amani na utulivu uliopo chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema kiwanda hicho pia ni ushahidi wa mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na China, huku akiwataka Watanzania kuendelea kulinda amani kwani ndiyo msingi wa maendeleo na uwekezaji nchini.
“Uwekezaji huu ni matokeo ya mazingira mazuri ya uwekezaji na amani iliyopo nchini. Tuendelee kuilinda amani yetu ili miradi mikubwa kama hii iendelee kuanzishwa na kuwanufaisha wananchi,” alisema Mwang’onda.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mwalimu Fakii Lulandala, amesema kiwanda hicho ndicho kikubwa zaidi cha kuchakata madini ya kinywe katika wilaya hiyo, na kwamba kitakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kupitia ajira, biashara na ongezeko la mapato ya Halmashauri na Serikali kwa ujumla.
Madini ya kinywe (Graphite) yana umuhimu mkubwa katika uchumi wa dunia wa sasa kutokana na matumizi yake katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme, vifaa vya kuhifadhi nishati, vilainishi vya mitambo, vifaa vya elektroniki, teknolojia za anga pamoja na tafiti mbalimbali za kisayansi.
Kuanzishwa kwa kiwanda hicho kunakuja wakati dunia ikielekea kuongeza matumizi ya nishati safi na kupunguza utegemezi wa nishati zinazochafua mazingira, jambo linaloifanya Tanzania kuwa sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani wa madini yanayohitajika katika teknolojia za kisasa.
Mradi huo unatajwa kuwa mfano halisi wa utekelezaji wa azma ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda unaotumia rasilimali za ndani, sambamba na maelekezo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayosisitiza kuongeza thamani ya madini na kuimarisha sekta ya viwanda kwa maendeleo endelevu.

