Na John Walter -Kiteto
Mwenge wa Uhuru 2026 umeweka jiwe la msingi la mradi mkubwa wa maji wa Nchinila hadi Engusero wenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 katika Kata ya Dosidosi, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, mradi unaotarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi ya 25,000 kutoka vijiji vinne kwa kuwapatia huduma ya maji safi na salama.
Mbali na kuwahudumia wananchi, mradi huo pia umezingatia sekta ya mifugo kwa kujenga birika maalumu la kunyweshea mifugo, hatua inayotarajiwa kupunguza migogoro ya matumizi ya maji kati ya binadamu na mifugo na kuimarisha shughuli za ufugaji katika eneo hilo.
Mradi huo unatekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kiteto, ukiwa sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuboresha upatikanaji wa huduma za maji vijijini.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, alisema ameridhishwa na maendeleo ya mradi huo, akieleza kuwa ni kielelezo cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
Alisema mradi huo unaendana na dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji, hatua itakayomtua mama ndoo kichwani, kuboresha afya za wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mwang’onda pia aliwataka wananchi kuutunza mradi huo na miundombinu yake ili uweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara, James Kionaumela, alisema mradi umefikia asilimia 75 ya utekelezaji na unaendelea vizuri kulingana na ratiba iliyopangwa, huku akieleza kuwa ukikamilika utaleta mabadiliko makubwa katika upatikanaji wa maji kwa wananchi wa eneo hilo.
Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Dosidosi wameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo, wakisema utamaliza adha ya muda mrefu ya ukosefu wa maji na kuboresha maisha yao pamoja na shughuli za uzalishaji, hususan ufugaji na shughuli nyingine za kiuchumi.

