Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mha. Wolta Kirita, amesisitiza umuhimu wa kushirikisha Vyombo vya Utoaji wa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) katika mipango na programu zote zinazolenga kuboresha huduma za maji vijijini ili kuhakikisha huduma hizo zinakuwa endelevu na wananchi wanaendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.
Mha. Kirita ametoa maelekezo hayo Julai 13, 2026, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kuhusu utekelezaji wa Programu ya Lipa kwa Matokeo (PforR II) Awamu ya Pili, yanayofanyika katika Ukumbi wa Rocky City Mall, jijini Mwanza. Mafunzo hayo yanawakutanisha waratibu wa programu kutoka Wizara za Maji, Afya, Elimu na TAMISEMI.
Akizungumza na Mameneja wa Mikoa (RMs) na Mameneja wa Wilaya (DMs), Mkurugenzi Mkuu aliwataka kuendelea kuzisimamia CBWSOs kwa ukaribu na kuhakikisha zinajengewa uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Alieleza kuwa RUWASA inaelekea kuanzisha mfumo wa mikataba ya utendaji kazi ili kuongeza uwajibikaji na kuondokana na utendaji wa mazoea (business as usual), kwa lengo la kujenga utamaduni wa matokeo.
«“RMs na DMs ninyi ndiyo DGs kwenye maeneo yenu. Mmepewa mamlaka ya kufanya maamuzi kwa niaba ya taasisi, hivyo yatumieni ipasavyo. Natamani kuona Makao Makuu yakijikita zaidi katika kazi za kimkakati, kama kutafuta programu mpya za maendeleo badala ya kushughulikia masuala ya kawaida ya usimamizi wa miradi,” alisema Mha. Kirita.»
Aidha, aliwataka viongozi hao kuendelea kuzisaidia CBWSOs kuandaa mipango bora ya uendeshaji na matengenezo, kuwajengea uwezo, kuhakikisha upatikanaji wa vipuri kupitia mfumo wa framework contracts, kuimarisha matengenezo kinga na kusimamia matumizi sahihi ya fedha ili kuhakikisha huduma za maji zinaendelea kuwa endelevu.
«“Uendelevu wa huduma za maji unategemea pia utunzaji wa vyanzo vya maji. Hili ni jukumu la kila mmoja wetu na tunapaswa kulisimamia kwa pamoja,” alisisitiza.»
Mkurugenzi Mkuu alisema muundo wa RUWASA umeendelea kuonesha ufanisi katika utoaji wa huduma za maji safi vijijini na kusisitiza kuwa wadau wote wanaotekeleza Programu ya PforR kutoka sekta mbalimbali wanapaswa kushirikiana kwa karibu ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.
Alibainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya Awamu ya Kwanza ya Programu ya PforR yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza kasi ya utekelezaji katika Awamu ya Pili itakayoanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Katika kuimarisha uendelevu wa huduma za maji vijijini, RUWASA imeendelea kutekeleza mkakati wa kuzijengea uwezo CBWSOs kupitia ukaguzi wa utendaji, mafunzo ya uendeshaji na matengenezo, pamoja na usimamizi unaolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

