Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Simeone Nyansaho, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza misingi ya uadilifu, haki na ushindani wa kweli katika Mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF Cup 2026), akisema misingi hiyo ndiyo itakayowezesha kupatikana kwa washindi wanaostahili na kuongeza hadhi ya mashindano hayo.
Akizungumza Julai 13, 2026 wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo, Dkt. Nyansaho amesema waamuzi, waandaaji na washiriki wote wanapaswa kuzingatia maadili ya michezo ili kuhakikisha ushindani unafanyika kwa uwazi, haki na bila upendeleo.
Waziri huyo pia ameliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda, kuendelea kutoa kipaumbele kwa michezo inayokuza na kuibua vipaji vinavyoweza kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa, hususan mchezo wa riadha na michezo mingine ya ushindani.
Amesema kaulimbiu ya mashindano hayo isemayo “Umoja, Amani na Mshikamano kwa Ujenzi wa Taifa Letu Imara” inalenga kuimarisha mshikamano miongoni mwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini.
Aidha, Dkt. Nyansaho amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda, kwa maandalizi mazuri ya mashindano hayo pamoja na kuendelea kuimarisha michezo ndani ya JWTZ, hatua ambayo imeongeza ushiriki wa kamandi mbalimbali na kutoa fursa ya kuibua vipaji vipya vya wanamichezo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda, amesema ana imani CDF Cup 2026 itaendelea kuwa chachu ya kuibua wanamichezo wenye uwezo mkubwa wa kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa na kuongeza idadi ya medali za dhahabu kupitia michezo mbalimbali.
Jenerali Mkunda amesema mashindano hayo pia yanalenga kuimarisha timu za michezo za JWTZ, kukuza nidhamu kwa wanamichezo pamoja na kuhakikisha sheria na kanuni za kila mchezo zinazingatiwa wakati wote wa mashindano.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF Cup 2026), Brigedia Jenerali Said Hamis Said, amesema mashindano hayo yameanza rasmi Julai 13 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 29, 2026, yakihusisha michezo mbalimbali ikiwemo riadha, kuogelea, mishale, ngumi na soka la ufukweni.
Brigedia Jenerali Said amesema pamoja na kuibua vipaji vya wanamichezo, mashindano hayo ni sehemu ya maandalizi ya ushiriki wa JWTZ katika mashindano ya kitaifa na kimataifa. Aidha, amewakaribisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo, akibainisha kuwa viingilio ni bure.

