Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Godfred Mbanyi, amesema Bodi hiyo imepata mafanikio makubwa kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), huku ikitumia fursa hiyo kuanza rasmi maandalizi ya Kongamano la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi la mwaka 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 13, 2026, jijini Dar es Salaam, katika banda la PSPTB lililopo ndani ya banda la Wizara ya Fedha kwenye maonesho hayo, Mbanyi amesema mwaka 2026 unaadhimisha miaka 10 mfululizo ya PSPTB kushiriki Maonesho ya Sabasaba.
Amesema maonesho ya mwaka huu yamekuwa na mafanikio makubwa, ambapo wadau mbalimbali wametembelea banda la PSPTB na kupata ufafanuzi kuhusu mitihani, taratibu za usajili pamoja na majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na bodi katika kuendeleza taaluma ya ununuzi na usimamizi wa mnyororo wa ugavi nchini.
Aidha, amebainisha kuwa PSPTB imezindua rasmi maandalizi ya Kongamano la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi litakalofanyika kuanzia Desemba 14 hadi 18, 2026, katika Hoteli ya Ngurudoto, mkoani Arusha.
Pia amesema kongamano hilo litawakutanisha wabobezi wa tasnia ya ununuzi na ugavi pamoja na wataalamu kutoka nyanja mbalimbali, ikiwemo maadili na afya, watakaowasilisha mada kwa lengo la kuendeleza na kuimarisha taaluma hiyo.
Mbanyi ameongeza kuwa mada kuu ya kongamano pamoja na mada ndogo zitakazowasilishwa zitatangazwa kupitia tovuti ya PSPTB ifikapo mwishoni mwa wiki, ili kutoa nafasi kwa wataalamu kujiandaa kuwasilisha kazi zao.
Amesema bodi inatarajia kupokea mawasilisho yatakayozingatia hali halisi ya utendaji wa mnyororo wa ugavi, maendeleo na mabadiliko yanayoendelea katika sekta hiyo, badala ya kuwasilisha nadharia pekee.
Aidha, amewataka wataalamu na wadau mbalimbali kuanza maandalizi ya kushiriki kongamano hilo, akibainisha kuwa kwa mara ya kwanza litafanyika kwa muda wa siku tano badala ya siku tatu.

