Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetambulisha rasmi mfumo mpya wa kufunga nyaya za umeme majumbani utakaowezesha wateja kufuatilia matumizi ya umeme kupitia simu ya mkononi. Mfumo huo unajulikana kama Smart House.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema hayo alipokuwa akieleza mambo muhimu aliyomweleza Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alipotembelea banda la TANESCO katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Twange amesema kupitia mfumo huo, mteja ataweza kuona kifaa gani ndani ya nyumba kinatumia umeme mwingi na kukizima akiwa popote alipo kupitia simu yake.

“Hata kama uko Mwanza au Dubai na nyumba ipo Kigoma, unaweza kuzima kifaa hicho ukiwa huko, hivyo kudhibiti matumizi ya umeme usiyoyahitaji,” amesema.

Ameeleza kuwa ubunifu huo umetokana na malalamiko ya wateja waliokuwa wakidai kuwa matumizi yao si makubwa, lakini umeme unaisha kwa haraka.

Aidha, amesema baadhi ya wateja walikuwa wakilalamikia mita kutosoma vizuri na hivyo kulazimika kuiomba TANESCO kufanya ukaguzi. Mfumo huo utasaidia kubaini kifaa kinachotumia umeme mwingi na kurahisisha ufuatiliaji wa matumizi.

Twange amesema teknolojia hiyo mpya inatarajiwa kuzinduliwa rasmi muda si mrefu kabla ya kusambazwa kwa wateja nchini, hatua inayoonyesha juhudi za wahandisi wa TANESCO katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili watumiaji wa umeme.

Amewahimiza wateja kuendelea kutoa maoni na changamoto zao, akieleza kuwa shirika linaendelea kubuni teknolojia na huduma mpya ili kuboresha huduma zake.

Pia alimshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa kutembelea banda la TANESCO na kupata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na shirika hilo.

Kwa upande wa nishati safi ya kupikia, Twange amesema alimweleza Rais kuhusu hatua zinazochukuliwa kutekeleza mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati hiyo.

Amesema kwa sasa TANESCO inaendelea na mpango wa Bill Financing, unaowezesha wateja wapya na waliopo kukopeshwa majiko ya umeme na kurejesha gharama zake taratibu kupitia ununuzi wa umeme.

“Mpango huu umepata mwitikio mzuri na umefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 90. Ndiyo maana tumehusisha sekta binafsi kupitia mikataba mbalimbali ili kuongeza upatikanaji wa majiko kwa wananchi,” amesema.

Ameongeza kuwa wananchi hawapaswi kuogopa kutumia umeme kwa kupikia, kwani tafiti za wahandisi na wanasayansi zimewezesha kutengenezwa kwa majiko yanayotumia umeme kwa ufanisi mkubwa na kwa gharama nafuu ikilinganishwa na nishati nyingine.

Kuhusu miundombinu ya umeme, Twange amesema alimweleza Rais Dk. Mwinyi kuhusu utekelezaji wa mradi mkubwa wa kujenga njia mpya za kusafirisha umeme kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar.

Amefafanua kuwa mradi huo utahusisha njia tatu za umeme zinazopita chini ya bahari: kutoka Dar es Salaam kwenda Unguja, kutoka Tanga kwenda Pemba, na kutoka Dar es Salaam kwenda Mafia.

Kwa mujibu wa Twange, mhandisi mshauri wa mradi anatarajiwa kupatikana mwezi Agosti, huku mkandarasi akitarajiwa kupatikana Januari. Utekelezaji wa mradi huo unakadiriwa kuchukua miezi kati ya 20 na 22.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uwezo wa kusafirisha umeme wa kutosha kwenda Zanzibar, jambo litakalokidhi mahitaji yanayoendelea kuongezeka kutokana na kasi ya maendeleo ya kiuchumi na ujenzi katika kipindi cha uongozi wa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi.