Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, (DITF) maarufu kama Sabasaba, yamekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kujifunza teknolojia mpya, kukuza biashara na kuimarisha ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 13 Julai 2026, alipoyafunga rasmi Maonesho ya Kimataifa ya Miaka 50 ya Biashara, jijini Dar es Salaam.
Amesema katika kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, Maonesho hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza diplomasia ya biashara na uchumi, ambapo wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani wamekuwa wakishiriki, kuwekeza na kutangaza huduma pamoja na bidhaa mbalimbali za kibiashara.
Ameeleza kuwa Maonesho hayo pia yamekuwa jukwaa muhimu kwa Watanzania kudhihirisha uwezo na utayari wao katika ubunifu na uzalishaji wenye tija, ikiwemo uzalishaji wa bidhaa bora na matumizi ya teknolojia za kisasa.
Aidha, amesema Maonesho hayo ni fursa muhimu ya kuimarisha uwezo wa Watanzania katika kujenga uchumi imara, wa kisasa na wenye ushindani, huku akisisitiza kuwa maendeleo ya Taifa yanategemea utekelezaji wa vipaumbele vya kitaifa kwa vitendo, nidhamu na uwajibikaji.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kusimamia na kuweka mazingira bora na wezeshi yatakayochochea matokeo chanya katika sekta za biashara na viwanda nchini kwa manufaa mapana ya Taifa.
Amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo kuwahamasisha Watanzania kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana, ikiwemo Soko Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA), kwa lengo la kuimarisha biashara na kuongeza masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
Rais Dkt. Mwinyi amewahamasisha wafanyabiashara kutumia fursa hizo kutangaza na kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania, huku akisisitiza kuwa taasisi za Serikali zina wajibu wa kuondoa urasimu unaokwamisha utoaji wa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi na wafanyabiashara.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kusimamia rasilimali za umma kwa uadilifu na uwajibikaji, pamoja na kuitaka TanTrade kuendelea kutafuta fursa mpya za masoko na kuhakikisha huduma wezeshi zinapatikana ili kuwasaidia Watanzania kunufaika na fursa hizo.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi amesema maendeleo ya Taifa yanahitaji amani, umoja na mshikamano, na kuwasisitiza wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuwa wamoja, kulinda amani ya nchi na kufanya kazi kwa bidii na uzalendo.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi alikabidhi tuzo maalum kwa washindi na washiriki waliofanya vizuri katika Maonesho ya mwaka 2026. Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ametunukiwa Tuzo Maalum ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, kwa kutambua ushiriki wake na mchango anaoendelea kutoa katika kufanikisha maonesho hayo.
Mapema, Rais Dkt. Mwinyi alitembelea mabanda mbalimbali ya Maonesho hayo na kujionea bidhaa na huduma zinazotolewa na taasisi za umma, sekta binafsi pamoja na washiriki kutoka mataifa mbalimbali waliohudhuria Jubilei ya Dhahabu ya miaka 50 ya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam.

