NA DENIS MLOWE,IRINGA 

MBUNGE wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, ameendelea kuunga mkono jitihada za maendeleo katika jimbo lake baada ya kukabidhi mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa nyumba ya watumishi katika Kijiji cha Magunga, Kata ya Maboga.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Kiswaga alisema mchango huo ni sehemu ya juhudi zake za kuhakikisha mazingira bora ya kazi yanapatikana kwa watumishi wanaohudumu katika eneo hilo.

Alisema tayari aliwahi kutoa bati 100 kwa ajili ya mradi huo na akaahidi kuendelea kushirikiana na wananchi hadi ujenzi utakapokamilika.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Magunga, Michael Mgimwa, alimpongeza Mbunge huyo kwa msaada alioutoa akieleza kuwa mifuko hiyo ya saruji itachochea kasi ya ujenzi wa nyumba hiyo

Alisema lengo la wananchi ni kuukamilisha mradi huo ifikapo mwezi Oktoba ili kupunguza changamoto zinazowakabili baadhi ya watumishi wanaolazimika kupanga nyumba kutokana na uhaba wa makazi.

Katika ziara hiyo, Mbunge Kiswaga pia alikutana na wananchi na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili, ambapo suala la migogoro ya ardhi lilijitokeza kuwa kero kubwa. Wananchi walieleza malalamiko yao kuhusu mwekezaji mmoja ambaye walidai amechukua sehemu ya ardhi yao kinyume na utaratibu, jambo walilosema limeathiri shughuli zao za kiuchumi na maisha yao ya kila siku.

 Waliiomba Serikali kulifuatilia suala hilo ili uchunguzi ufanyike na haki itendeke kwa pande zote.

Akijibu hoja hizo, Kiswaga aliwahakikishia wananchi kuwa atalifuatilia kwa karibu kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika ili kuhakikisha linapatiwa ufumbuzi kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.