Na Mwandishi wetu, Mirerani
MWENGE wa uhuru umeanza mbio zake mkoani Manyara huku ukitarajiwa kupitia, kukagua, kuweka jiwe la msingi na kuzindua miradi 49 ya thamani ya shilingi bilioni 139.
Mwenge wa uhuru umepokelewa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro ukitokea mkoani Arusha na unatarajiwa kukabidhiwa mkoani Singida Julai 18, 2026 ili kuendelea na mbio zake.
Kaimu mkuu wa mkoa wa Manyara, Halima Dendegu ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Singida amekabidhiwa na mkuu wa mkoa wa Arusha, Amos Makala amesema mwenge huo wa uhuru utakimbizwa katika halmashauri saba za Manyara.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala amesema ukiwa eneo hilo unatarajiwa kukimbizwa kilomita 238 na kupitia miradi saba ya thamani ya Sh57.2 bilioni.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2026 Wazo Mwang’onda akizungumza wakati akikagua miradi mbalimbali ya maendeleo ameiasa jamii kutunza amani.
“Hawa wawekezaji wametoka China na kuwekeza hapa Tanzania kwa sababu ya amani iliyopo kwani kungekuwa na vurugu ingekuwa tatizo hivyo amani iliyopo itunzwe,” amesema Mwang’onda.
Amempongeza mkurugenzi wa kampuni ya Chusa Mining LTD Joseph Mwakipesile kwa kutumia Sh230 milioni kujenga wodi mbili za wanawake na watoto na ofisi ya wauguzi katika kituo cha afya Mirerani.
Mkurugenzi wa Chusa Mining LTD, Joseph Mwakipesile amesema wamewiwa kusaidia jamii baada ya kusikia changamoto ya wodi ya wanawake na watoto ili kurudisha kidogo wanachopata kwa watu.
Mkimbiza mwenge wa uhuru kitaifa Inyasi Amsi kutoka mkoa wa Manyara, amewashukuru viongozi na wananchi wa Manyara kwa kumlea vyema hadi kupata nafasi hiyo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki James Ole Millya ambaye pia ni mbunge wa Simanjiro amepongeza kampuni ya wachina Permanent Minerals kuwekeza katika madini ya kinywe kijiji cha Kandasikira kata ya Shambarai.
Mwakilishi wa Permanent Minerals Elisha Mnyawi amesema wanazalisha tani 6,000 kila mwezi za madini ya kinywe na kuziuza katika mataifa mbalimbali ikiwemo Maremani, China na India.
Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mirerani, Dkt Namnyaki Lukumay amesema wodi hizo za wanawake na watoto zilizojengwa na Chusa Mining zitaondoa changamoto ya uchache wa vyumba hivyo.
Mkurugenzi wa J. N Mining LTD, Justin Nyari amesema viongozi wa mwenge wa uhuru wamepanda miti katika shule ya awali na msingi Glisten ili kutunza mazingira.
