…………
Happy Lazaro ,Arusha .
Arusha .Katibu Mkuu wa Taasisi ya Twariqa, Sheikh Haruna Husein, amesema Taasisi hiyo imemwandikia rasmi barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikimuomba kuwa mgeni rasmi na kuongoza dua maalumu ya kuliombea Taifa itakayofanyika Agosti 21 mwaka huu katika Zawiya Kuu ya taasisi hiyo jijini Arusha.
Sheikh Haruna amesema dua hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya aliyekuwa Kiongozi wa Taasisi ya Twariqa, Hayati Daruweshi Mtimkavu, ambaye alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha mafundisho ya dini, amani na mshikamano wa Watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Zawiya Kuu ya Taasisi ya Twariqa mkoani Arusha, amesema maandalizi ya shughuli hiyo yamekamilika na waumini pamoja na wageni kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wanatarajiwa kushiriki kwa wingi katika ibada hiyo ya kitaifa.
Ameeleza kuwa ratiba ya siku hiyo itaanza mchana kwa programu maalumu ya kinamama itakayojumuisha mawaidha na dua, huku shughuli kuu ikiendelea usiku kucha kwa ibada, dhikri, maombi na dua mbalimbali hadi alfajiri kwa lengo la kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani, umoja na maendeleo.
Kwa mujibu wa Sheikh Haruna, maadhimisho hayo yana historia ndefu tangu mwaka 1972, ambapo viongozi mbalimbali wa kitaifa wamekuwa wakishiriki katika dua hizo, wakiwemo Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete.
Amesema iwapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atashiriki katika dua hiyo, itakuwa ni ishara ya kuendeleza mshikamano wa kitaifa na kuthamini nafasi ya dini katika kuhimiza amani, upendo na maadili mema nchini.
Aidha, ametoa wito kwa waumini wa dini pamoja na wananchi wote wenye mapenzi mema na Taifa kujitokeza kushiriki katika dua hiyo, akisisitiza kuwa maombi ya pamoja yana nafasi muhimu katika kuiombea Tanzania iendelee kuwa salama, yenye umoja, utulivu na maendeleo endelevu.
“Dua hii inalenga kumuombea Hayati Daruweshi Mtimkavu, ambaye aliacha urithi wa upendo, umoja na maridhiano, lakini pia kuliombea Taifa letu liendelee kuwa na amani, utulivu na mshikamano,” amesema Sheikh Haruna.
“Amani ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa, akibainisha kuwa viongozi wa dini wana wajibu wa kuendelea kuhubiri, kuilinda na kuikuza kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.”amesema Sheikh Haruna .
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana Taifa kupitia Taasisi ya Twariqatul Qadiriyya Arraziqiyya Al-Jaylaniyya, Khalifa Juma Salim, amewahimiza vijana na Watanzania kwa ujumla kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano, akieleza kuwa utulivu ndiyo msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Khalifa amewataka wananchi kuepuka vitendo vya vurugu na migawanyiko, huku akisisitiza umuhimu wa kushikamana na mafundisho ya Qur’ani na Sunnah pamoja na kuenzi maadili mema.
Naye Kiongozi wa Taasisi ya Twariqatul Qadiriyya Wilaya ya Arumeru, Sheikh Iddy Ngella, amesema Watanzania wanapaswa kuendelea kushikamana, kusikilizana na kuheshimiana ili kulinda amani na utulivu wa Taifa.
“Tunapaswa kushikamana, kusikilizana na kuheshimiana ili Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani,” amesema Sheikh Ngella.

