Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, ameongoza uzinduzi wa mazoezi ya pamoja kupitia NJE Jogging Club. Hatua hiyo inalenga kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi miongoni mwa watumishi wa Wizara ili kuimarisha afya, ustawi, na ufanisi kazini.
Mazoezi hayo ya kwanza yamewakutanisha watumishi wa Wizara katika mbio za pamoja eneo la Mtumba jijini Dodoma. Huu ni mwanzo wa programu endelevu itakayokuwa ikifanyika kila siku ya Jumanne na Alhamisi, kuanzia saa 10:30 jioni, kwa lengo la kuhamasisha maisha yenye afya, kuongeza utimamu wa mwili na akili, pamoja na kuimarisha mshikamano mahali pa kazi.
Akizungumza kuhusu mpango huo, Kocha wa NjeJogging Club, Shabani Maganga, ameeleza kuwa uwekezaji katika afya ya watumishi ni sehemu muhimu ya kuongeza ari ya kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kupitia kaulimbiu ya “Afya Yako, Utendaji Wako,” Wizara inaendelea kuhimiza watumishi wake kushiriki kikamilifu katika mazoezi hayo, ikitambua kuwa afya bora ndiyo msingi wa utendaji wenye tija na mafanikio ya taasisi.

