TAARIFA KWA UMMA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa taarifa kuhusiana na ajali iliyotokea mnamo tarehe 09 Julai, 2026 saa 1:45 usiku huko maeneo ya Mambi Kata ya Kongolo Mswiswi Wilaya ya Mbarali katika Barabara Kuu ya Mbeya Njombe.

Ni kwamba gari aina ya Toyota Landcuiser lenye namba ya usajili DFPB 1165 mali ya Wizara ya Kilimo-Mkoa wa Njombe lililokuwa likitokea Njombe kuelekea Mbeya likiendeshwa na Dereva aitwaye Christopher Rwegasira liligonga kwa nyuma gari namba T.266 DJU mali ya Kampuni ya Motema MP Limited likiendeshwa na Dereva aitwaye Frank Julius lililokuwa likitokea Njombe kuelekea Mbeya na kisha tena kuligonga gari namba T.882 BFC aina ya Mitsubish Fuso lililokuwa likiendeshwa na Dereva aitwaye Nicko Shabani na kusababisha Kifo kwa abiria aliyekuwa kwenye gari namba DFPB 1165 aitwaye Peter Jackson, Afisa Kilimo Nyanda za Juu Kusini.

Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa gari namba DFPB 1165 Toyota Landcuiser kushindwa kuchukua tahadhari wakati akitaka kulipita (Overtaking) gari lililokuwa mbele yake. Aidha mara baada ya ajali hiyo Dereva wa gari namba DFPB 1165 alikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Inyala Mbeya kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu huku jitahada za kumtafuta dereva wa gari namba DFPB 1165 zikiendelea.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa Madereva kuzingatia Sheria za Usalama barabarani ili kuepuka ajali ambazo zinaepukika.