Na Mwandishi wa OTR
Kibaha, Pwani. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) imejiwekea lengo la kukusanya Sh2 trilioni kama mapato yasiyo ya kodi katika mwaka huu wa fedha 2026/27, ikiwa ni zaidi ya lengo la Sh1.79 trilioni ambalo Serikali imeipa taasisi hiyo.
Akifungua Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi wa OTR uliofanyika Alhamisi, Julai 9, 2026, wilayani Kibaha, mkoani Pwani, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema kufikiwa kwa lengo hilo kutategemea kuongeza kasi ya utendaji, ubunifu, ushirikiano na uwajibikaji ndani ya OTR na katika taasisi na kampuni 308 zinazosimamiwa na ofisi hiyo.
“Ili tuweze kufikia lengo letu la kukusanya Sh2 trilioni katika mwaka wa fedha 2026/27, itatubidi tutanue mbavu na kutoa jasho zaidi,” alisema Bw. Mchechu.
Alisisitiza kuwa mafanikio hayo yatawezekana ikiwa OTR itaendelea kujenga mazingira bora ya kazi, kuimarisha utamaduni wa taasisi unaovutia na kuhifadhi watumishi wenye uwezo, sambamba na kuhakikisha uwekezaji wa Serikali wenye thamani ya Sh92.3 trilioni unazalisha matokeo yanayoonekana kwa wananchi.
Katika mwaka wa fedha 2025/26, OTR ilikusanya Sh1.327 trilioni kama mapato yasiyo ya kodi, ikiwa ni ongezeko la asilimia 30 kutoka Sh1.028 trilioni zilizokusanywa mwaka 2024/25.
Kati ya kiasi hicho, gawio lilichangia Sh800.5 bilioni, sawa na asilimia 60 ya makusanyo yote; michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi kutoka taasisi za umma zisizo za kibiashara ilifikia Sh406 bilioni, sawa na asilimia 30 ya makusanyo; huku mapato mengineyo, yakiwemo faida za uwekezaji na michango mingine inayotokana na umiliki wa Serikali, yakifikia Sh121.5 bilioni, sawa na asilimia 10 ya makusanyo yote.
“Wajibu wetu sasa ni kulinda mafanikio haya na kutoridhika na tulipofika. Tunapaswa kuhakikisha OTR inakuwa taasisi yenye uwezo na utayari wa kutekeleza wajibu wake mkubwa zaidi katika kusimamia uwekezaji wa umma na kuchangia utekelezaji wa Dira 2050,” alisema.
Alisema tangu kuanza kwa mwaka mpya wa fedha Julai 1, 2026, matarajio ya Serikali, wananchi na wadau kuhusu mchango wa OTR katika uchumi yameongezeka.
“Ofisi ya Msajili wa Hazina ina ahadi na wajibu mkubwa kwa Serikali wa kuvuka viwango vya sasa vya gawio na michango, kuendelea kuongeza thamani ya uwekezaji wa Serikali na kuhakikisha mapato yasiyo ya kodi yanaendelea kukua,” alisema.
Bw. Mchechu alisema azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuongeza mchango wa mapato yasiyo ya kodi hadi kufikia asilimia 10 ya mapato yote ya Serikali ifikapo mwaka 2030, kutoka wastani wa sasa wa takribani asilimia tatu.
Alisema kufikia lengo hilo kutahitaji taasisi zinazosimamiwa na OTR kuongeza tija, ufanisi na mapato, kuimarisha nidhamu ya kifedha, kupunguza utegemezi usio wa lazima kwa Serikali, pamoja na OTR yenyewe kuongeza ubora, kasi na ufanisi wa usimamizi wake.
“Hii ni ahadi kubwa, na utekelezaji wake unategemea mchango wa kila mmoja wetu,” alisisitiza.
Aliwataka watumishi kuongeza ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao, kufanya kazi kwa kasi, ubora na ufanisi, kutumia teknolojia na takwimu kufanya maamuzi bora, kuimarisha utamaduni wa uwajibikaji na ushirikiano, kuendelea kujifunza na kujenga uwezo, pamoja na kusimamia kwa uadilifu matumizi ya rasilimali za umma.
“Kila mtumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina anapaswa kuona uhusiano wa moja kwa moja kati ya kazi anayofanya na matokeo yanayotarajiwa na Taifa,” alisema.
Akizungumza Juni 30, 2026, wakati wa kupokea gawio na michango ya Sh1.327 trilioni kutoka OTR, Rais Dkt. Samia aliitaka taasisi hiyo kuhakikisha mashirika na taasisi za umma zinaongeza tija, ufanisi na ushindani, huku zikipunguza utegemezi wa ruzuku za Serikali na kuimarisha uwezo wa kujitegemea kifedha.
“Mafanikio haya yasitufanye turidhike. Uwekezaji wa umma ni mkubwa na matarajio ya wananchi ni makubwa zaidi,” alisema Rais Samia.
Alionya kuwa taasisi zinazofanya vizuri zisifiche udhaifu wa zile zinazosuasua.
“Kila taasisi iliyokabidhiwa mali za umma inapaswa kujieleza kwa lugha ya matokeo: imezalisha nini, imeongeza thamani kiasi gani, imechangia mapato kiasi gani, na imepunguza kwa kiwango gani utegemezi wake kwa Serikali,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango, Utafiti na Maendeleo wa OTR, Bw. Emanuel Luvanda, alisema utekelezaji wa Mpango Mkakati wa OTR wa mwaka 2026/27–2030/31 utaweka mkazo katika kuimarisha utawala bora, uongozi na usimamizi wa rasilimali watu, usimamizi wa utendaji, uhamasishaji wa rasilimali, kuboresha uwekezaji, ushirikishwaji wa wadau na kuijengea taasisi uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Aliyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 pamoja na vipaumbele vya Mpango Mkakati wa OTR mbele ya Baraza la Wafanyakazi.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bw. Chacha Marigiri, alisema OTR itaendelea kuwawezesha watumishi kuongeza elimu na ujuzi kupitia mafunzo na kujiendeleza kimasomo ili kuboresha utendaji na kuongeza tija.
“Tutaendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa watumishi wetu,” alisema, huku akisisitiza kuwa hakutakuwa na nafasi kwa watumishi wavivu na wazembe.
