……………..

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Bw. Othman Masoud Othman, amesema kutiwa saini kwa makubaliano ya maridhiano kati ya ACT Wazalendo na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni hatua muhimu ya kujenga Zanzibar yenye umoja, utulivu wa kisiasa na maendeleo ya kudumu, akisisitiza kuwa mchakato huo haukusudii kunufaisha vyama vya siasa pekee bali wananchi wote.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa maridhiano iliyofanyika Ikulu Zanzibar leo Julai 9, 2026, mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Marais Wastaafu wa Zanzibar, viongozi wa vyama vya siasa, mabalozi na wageni mbalimbali, Othman alisema mazungumzo yaliyoanza Novemba 9, 2021 yameweka msingi wa kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto za kisiasa zilizojitokeza baada ya uchaguzi.

“Nchi nyingi zilizopiga hatua ya maendeleo zimejenga kwanza mshikamano wa kijamii, utawala wa sheria, uwajibikaji, utulivu wa kisiasa na amani endelevu. Haya ndiyo tunayotafuta kwa Zanzibar kupitia maridhiano haya,” alisema.

Alieleza kuwa hatua zinazofuata zitahusisha kuundwa kwa kamati ya pamoja itakayochambua maeneo yote yaliyokubaliwa na kupendekeza namna ya kuyafanyia kazi, huku tume ya utekelezaji itakayoundwa kwa mujibu wa sheria ikisimamia utekelezaji wa makubaliano hayo.

Kwa mujibu wa Othman, maeneo yatakayopatiwa kipaumbele ni pamoja na kujenga imani na kuaminiana, kupitia upya Katiba, mfumo wa uchaguzi, utumishi wa umma, mfumo wa utoaji haki na serikali za mitaa ili kuimarisha utawala bora na ufanisi wa taasisi za umma.

Alisisitiza kuwa si sahihi kutafsiri maridhiano hayo kama suluhisho la kisiasa pekee kwa manufaa ya vyama vinavyoshiriki, bali ni mkakati wa muda mrefu wa kujenga mazingira bora ya kiuchumi, kijamii na kitaasisi yatakayoiwezesha Zanzibar kufikia ndoto yake ya kuwa kitovu cha biashara, huduma na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Hatua hizi si kwa faida ya vyama vya siasa tu. Ni kwa manufaa mapana ya Zanzibar na vizazi vijavyo. Tunajenga taasisi imara, uchumi wenye ushindani na mfumo wa haki utakaoweka mazingira bora ya uwekezaji na maendeleo,” alisema.

Othman pia alikiri kuwa bado yapo makundi yenye mitazamo tofauti kuhusu mchakato huo. Alisema kundi kubwa linaunga mkono maridhiano na lina matumaini makubwa, jingine limekata tamaa kutokana na historia ya utekelezaji wa makubaliano yaliyopita, huku kundi dogo likipinga kabisa juhudi hizo.

Aliwataka viongozi wa kisiasa, dini na jamii kushirikiana kujenga imani kwa wananchi ili kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kwa uaminifu na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

“Hawa waliokata tamaa wana hoja kutokana na walikotoka, lakini wakiona dhamira ya kweli watakuwa sehemu ya mafanikio ya mchakato huu. Wanaopinga kabisa ni wachache, lakini hatupaswi kuwapa nafasi ya kuzuia mustakabali wa Zanzibar,” alisema.

Katika hotuba yake, Othman alimshukuru Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuongoza mchakato huo kwa busara, pamoja na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za maridhiano na kuhimiza viongozi kusikiliza hata yale ambayo hayasemwi wazi.

Aidha, aliwashukuru viongozi mbalimbali walioshiriki kusimamia mazungumzo hayo tangu yalipoanza, akisema mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya hekima, uvumilivu na uzalendo wa pande zote zilizohusika katika kutafuta mustakabali mwema wa Zanzibar.