Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, leo ametembelea banda la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.
Katika ziara hiyo, Waziri alipokelewa na Mkuu wa Kitengo cha Habari wa NHC, Bw. Yahya Charahani, pamoja na timu ya Sabasaba ya Shirika, ambapo alipata fursa ya kujionea miradi mbalimbali ya makazi, biashara na matumizi mchanganyiko inayotekelezwa na NHC katika maeneo mbalimbali nchini, pamoja na fursa za uwekezaji zinazotolewa na Shirika.
Akipatiwa maelezo ya kina kuhusu maendeleo ya miradi hiyo, Mhe. Dkt. Akwilapo alieleza kufurahishwa na kiwango kikubwa cha uwekezaji kinachofanywa na NHC, akisema umefungua fursa nyingi za makazi, biashara, ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
“Mmefanya kazi kubwa sana. Miradi hii inaonesha uwezo mkubwa wa Shirika katika kuendesha uwekezaji wenye tija na kuleta manufaa kwa Watanzania,” alisema.
Waziri huyo pia aliipongeza NHC kwa kuendelea kujiendesha kwa ufanisi wa kibiashara, akibainisha kuwa Shirika ni miongoni mwa taasisi za umma zinazofanya vizuri na kujiendesha kwa nguvu zake, tofauti na baadhi ya taasisi zilizoshindwa kuhimili ushindani na kupoteza nafasi yake katika uchumi wa Taifa.
Aidha, aliisifu NHC kwa uwezo wake wa kutekeleza miradi mikubwa bila kutegemea ruzuku ya Serikali.
“Miradi yote hii mnajitegemea wenyewe; hamtegemei tena Serikali. Hiki ni kitu kikubwa sana. Hongereni sana kwa mafanikio haya,” alisisitiza.
Sambamba na pongezi hizo, Mhe. Dkt. Akwilapo aliitaka NHC kuendelea kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato na madeni yake kwa kuzingatia sheria na taratibu, akisisitiza kuwa hakuna mdaiwa anayepaswa kupewa upendeleo.
“Msitishike linapokuja suala la kudai malipo yenu halali. Hakuna mdaiwa anayepaswa kuogopwa. Wote wapeni ankara zao za madeni kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo,” alisema.
Aliongeza kuwa uwekezaji mkubwa unaofanywa na NHC umeendelea kuongeza upatikanaji wa makazi bora, fursa za biashara, ajira na uwekezaji, hivyo kuliagiza Shirika kuendelea na kasi hiyo ya ubunifu na utekelezaji kwa manufaa ya Watanzania.
Shirika la Nyumba la Taifa linaendelea kuwakaribisha wananchi kutembelea banda lake lililopo Mtaa wa Biashara ndani ya Viwanja vya Sabasaba ili kupata taarifa kuhusu miradi ya makazi, biashara, upangishaji, ununuzi wa nyumba na fursa mbalimbali za uwekezaji zinazotolewa na Shirika.
Karibu NHC Sabasaba – Tujenge Taifa Letu Pamoja.

