Mkuu wa wilaya ya Lindi Mhe. Victoria Mwanziva amewataka wanafunzi 60 watakaonufaika na mafunzo ya ufundi kupitia ‘Mradi wa Dumisha Amani’ unaofadhiliwa na mashirika ya kimataifa ya UNPDF, UNDP-Tanzania na kampuni ya CPP kuunda vikundi vya stadi zoa ili iwe rahisi kwa Serikali kuweza kuwapatia mikopo. 

Mwanziva amaetoa maagizo hayo tarehe 4 Julai, 2026 wakati wa hafla fupi ya ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo katika Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Lindi.

“Tuna vikundi vya vijana, vikundi vya maendeleo, karibuni sana Halmshauri tuna mikopo ya manispaa na ile ya asilimia 10 ya vijana, wanawake, wazee na wenye mahitaji maalum. Mikopo hii mtaipata mkiwa kwenye vikundi, ni rahisi kwani tayari mtakuwa na ujuzi na mkiwa na mpango unaotekelezeka mtaweza kunufaika na mikopo hii moja kwa moja,”amesema Mwanziva.

Mwanziva amewapongeza VETA, UNDPF, CPP, UNDP GPF-Tanzania kwa kuwezesha vijana kupata ujuzi kwa vitendo, stadi za maisha, ujasiriamali ili waweze kujiajiri au kujiriwa na kujikwamua kiuchumi. 

Kwa upande wake Afisa Mkuza Mitaala Mwandamizi kutoka VETA Makao Makuu, Alphoncina James Mshana amesema nafasi waliyoipata vijana hao ni ya kipekee na yenye thamani kubwa, hivyo amewahimiza kuitumia kikamilifu kwa kuhudhuria mafunzo yote, kuzingatia nidhamu, kufuata maelekezo ya wakufunzi na kushirikiana vizuri katika kipindi chote cha mafunzo.

Naye Josphine Sepeku, Afisa Mradi wa Dumisha Amani kutoka UNDP-Tanzania amesema wataendelea kusaidia vijana wa Tanzania kupata mafunzo ambayo yanawapa stadi na maarifa ya kujitegemea, hivyo kuchangia katika kudumisha amani.

 Aidha Mkuu wa chuo hicho, Harry Mmari amesema wanafunzi hao watapatiwa mafunzo ya vitendo katika stadi za Ufundi Umeme; Mapishi na Huduma za Hoteli; Ubunifu Ushonaji na Teknolojia ya Nguo; pamoja na Ufundi Bomba na hivyo ujuzi watakaoupata utakuwa mtaji muhimu wa maisha yao na msingi wa kujiletea maendeleo binafsi, ya familia zao na ya Taifa kwa ujumla.