‎Na Prisca Libaga  RS  Arusha
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Rasilimali Watu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Polycarp Nkuyuba, amewapa wanafunzi wa Chuo cha Dar es Salaam School of Journalism (DSJ) maelezo kuhusu muundo na mgawanyo wa kiutendaji wa Serikali, kuanzia ngazi ya Serikali za Mitaa hadi Serikali Kuu, pamoja na namna huduma zinavyowafikia wananchi.
‎Kuyuba ametoa maelezo hayo wakati wa ziara ya mafunzo ya wanafunzi hao katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Julai 03, 2026. Ziara hiyo imelenga kuwapatia wanafunzi uzoefu wa vitendo kuhusu utendaji wa Serikali na mawasiliano ya umma, hususan namna Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inavyotekeleza majukumu yake ya kila siku.
‎Aidha, wanafunzi hao wamepata fursa ya kujifunza utendaji wa Kitengo cha Habari, Mawasiliano na TEHAMA, ikiwemo namna taarifa rasmi za Serikali zinavyoandaliwa na kusambazwa kwa umma.
‎Ziara hiyo pia inalenga kuwaongezea ujuzi wa vitendo katika ukusanyaji wa taarifa, uandishi wa habari na matumizi ya mawasiliano ya umma ndani ya taasisi za Serikali.
‎Katika kipindi cha mafunzo, wanafunzi wanatarajiwa kupata nyaraka mbalimbali za kujifunzia, zikiwemo taarifa za Mkoa wa Arusha, rasimu za hotuba pamoja na taarifa rasmi za habari zinazotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

‎Uongozi wa Chuo cha Dar es Salaam School of Journalism (DSJ) umeeleza kuwa mafunzo ya vitendo ni sehemu muhimu ya kuwaandaa wanafunzi kwa kuwajengea ujuzi, weledi na uzoefu utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi watakapohitimu masomo yao.