Na. Saidina Msangi na Asia Singano, WF, Dodoma

Wananchi hususan vijana, wanawake na wajasiriamali wanaochipukia, wamehimizwa kutembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ili kujipatia elimu kuhusu huduma zinazotolewa na Wizara pamoja na Taasisi zake na kujionea fursa za kiuchumi na uwekezaji zinazochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Rai hiyo ilitolewa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati akizungumza na vyombo vya habari alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yenye Kaulimbiu kuu “Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba ni Fahari ya Tanzania”, yanayofanyika katika viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Mhe. Balozi Omar, alisema kupitia maonesho hayo ambayo yameendelea kuwa bora kila mwaka wananchi watakaotembelea Banda hilo watapata maelezo ya kina yatakayoridhisha kuhusu huduma za Wizara na fursa zilizopo kwa ajili yao.

“Tunategemea wananchi watakaotembelea Banda la Wizara ya Fedha wataridhika na maelezo haya ya namna idara zinavyotekeleza majukumu yake, pamoja na fursa zilizopo kwa wananchi, hasa vijana, watu wanaofungua biashara, na wanawake hivyo natoa rai kwa Watanzania wote kutembelea Banda letu,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aidha, Balozi Omar alisema kuelekea utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 inayolenga kufikia uchumi wa Dola trilioni moja kufikia 2050, Tanzania inahitaji uwekezaji mkubwa ili kukuza uchumi wa sasa ambapo nguvu kubwa inatakiwa itoke kwenye uwekezaji wa ndani ili umiliki wa uchumi wa nchi ubaki mikononi mwa Watanzania wenyewe.

“Tunategemea ukuzaji huu wa uchumi utokane na uwekezaji mkubwa wa Watanzania wenyewe kuwekeza kwenye fursa zilizopo, ili wale wawekezaji wa nje wakija wakute tayari tunaendelea ili umiliki wa uchumi wetu sehemu kubwa utokane na uwekezaji wa ndani,” alisisitiza Balozi Omar.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa Dira ya 2050 unatarajiwa kuchukua kipindi cha miaka 25, ukiwa umegawanywa katika awamu za miaka mitano mitano ambapo utekelezaji umeanza rasmi Julai moja mwaka huu ukiongozwa na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

Aidha, Balozi Omar alitoa rai kwa Watanzania kuchangamkia fursa zinazotokana na miradi ya kimkakati iliyotajwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi hiki cha miaka mitano hadi 2030 ambapo Serikali imepanga kufanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya miundombinu na nishati.

‘‘Mbali na kukamilisha reli ya SGR inayoendelea sasa, Serikali imepanga kujenga njia mpya mbili za kimkakati kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay, na kutoka Tanga kupitia Arusha hadi Musoma,’’alifafanua Balozi Omar.

Aliongeza kuwa Serikali inalenga kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme kutoka megawati zaidi ya 4,000 za sasa na kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030, kuendeleza miradi mikubwa ya maji, mtandao wa Taifa wa maji, miradi ya umwagiliaji, Barabara pamoja na mawasiliano ili kufungua fursa zaidi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Mhe. Balozi Omar alitoa rai kwa Watanzania wote kuchangamkia fursa zinazopatikana katika utekelezaji wa miradi hiyo na kuwa sekta ya fedha iko tayari kuwawezesha mitaji wale wenye nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali.