Na Ashrack Miraji 

SAME, Kilimanjaro, Juni 28 — Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Wazo Mwang’onda, ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 2.159 iliyotembelewa katika Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2026.

Mwenge wa Uhuru uliwasili mkoani Kilimanjaro leo ukitokea Mkoa wa Tanga na kupokewa katika Kata ya Hedaru, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, alimkabidhi Mwenge huo Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Godfrey Mzava, kwa ajili ya kuendelea na mbio zake ndani ya wilaya hiyo.

Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mhe. Godfrey Mzava alisema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa umbali wa kilomita 76 katika Wilaya ya Same na utapitia miradi mitano ya maendeleo yenye thamani ya jumla ya Shilingi bilioni 2.159 kwa ajili ya kukaguliwa, kuwekwa mawe ya msingi, kuzinduliwa na kutembelewa.

Katika ziara hiyo, Mwenge wa Uhuru ulikagua miradi ya afya, miundombinu, miradi ya kijamii, vikundi vya wajasiriamali pamoja na kuzindua jukwaa (platform) la vijana la Wilaya ya Same, hatua inayolenga kuimarisha ushiriki wa vijana katika shughuli za maendeleo na kujenga uchumi wa wilaya hiyo.

Miongoni mwa miradi iliyopongezwa ni ujenzi wa wodi mbili za wagonjwa, za wanawake na wanaume, pamoja na jengo la kuhifadhia miili katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Same, ambapo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa aliweka jiwe la msingi na kupongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wake.

Ndugu Wazo Mwang’onda alisema ameridhishwa na ubora wa miradi hiyo na kusisitiza kuwa inakwenda kuongeza thamani ya huduma kwa wananchi. Aidha, aliwataka wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha kazi zilizobaki kwa kuzingatia viwango vya ubora, muda wa mkataba na matumizi sahihi ya fedha za umma.

Alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo ili kuboresha maisha ya wananchi, hivyo ni wajibu wa viongozi, wataalamu na wananchi kulinda na kuitunza miradi hiyo ili iweze kutoa huduma kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Godfrey Mzava, alimshukuru Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo, akisema maoni na ushauri uliotolewa utakuwa chachu ya kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi ya maendeleo wilayani humo.

Mhe. Mzava alisisitiza kuwa uongozi wa Wilaya ya Same utaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazokusudiwa na Serikali, huku akiahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuharakisha maendeleo ya wilaya hiyo.

Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Same walieleza kufurahishwa na kukamilika kwa baadhi ya miradi hiyo, wakisema itaongeza upatikanaji wa huduma muhimu hususan katika sekta ya afya. Mkazi wa Same, Hawa Said, alisema ujenzi wa wodi mpya na majengo ya kuhifadhia miili utasaidia kuboresha huduma hospitalini na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika kutokana na changamoto za miundombinu.

Baada ya kukamilisha mbio zake ndani ya Wilaya ya Same, Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kukabidhiwa kesho kwa wilaya inayofuata kwa mujibu wa ratiba ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, huku viongozi wakitoa wito kwa wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika kulinda amani, kuchochea maendeleo na kuunga mkono miradi inayotekelezwa na Serikali.

Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2026 Tanzania ni Yetu Sote tushikamane Kwa pamoja kuleta Maendeleo