Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesema ujenzi wa Bwawa la Farkwa ni mradi wa kimkakati unaolenga kutoa suluhisho la kudumu la changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dodoma na maeneo ya jirani. Amesisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati, kwa ubora na kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha ili wananchi waanze kunufaika na matokeo yake kwa haraka.

Aidha, Waziri Aweso amemtaka mkandarasi kutekeleza mradi kwa kuzingatia masharti ya mkataba na viwango vya kitaalamu, huku akizitaka taasisi zote zinazohusika kusimamia utekelezaji wa mradi huo kufanya kazi kwa ushirikiano na uwajibikaji ili kuhakikisha hakuna ucheleweshaji unaoweza kuathiri malengo ya Serikali ya kuboresha huduma ya maji.

Vilevile, ameeleza kuwa kukamilika kwa Bwawa la Farkwa kutaimarisha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Dodoma, sambamba na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ufugaji wa samaki, kuongeza usalama wa chakula na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika.