Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
WANACHAMA wapya 165 wamejiunga na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kibaha Mjini, Mkoa wa Pwani, hatua inayoonesha mwitikio wa wanawake kushiriki katika umoja huo.
Wanachama hao wametoka katika kata tatu, ambapo Tumbi wamejiunga wanachama 65, Kongowe 50 na Maili Moja 50.
Katibu wa UWT Kibaha Mjini, Cecilia Ndallu, anaeleza kuwa kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu, idadi ya wanachama wa jumuiya hiyo ilikuwa imefikia 35,844, hivyo baada ya ongezeko la wanachama hao 165 idadi itafikia 36,009.
Aidha ameeleza UWT Kibaha Mjini imefanikiwa kujenga ofisi katika kata tano kati ya kata 14 zilizopo, hatua inayolenga kuimarisha utendaji kazi wa jumuiya hiyo.
Vilevile amewahimiza wanawake wengine kuendelea kujiunga na umoja huo ili kuwa sehemu ya jukwaa la kushirikiana, kujifunza na kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Ndallu amewataka wanachama kulipa ada kwa wakati, huku akiwaomba kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kueleza mafanikio ya mageuzi makubwa ya maendeleo yanayofanyika kupitia sekta mbalimbali ikiwemo afya, maji, elimu na miundombinu.
Amewahimiza kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili kutumia fursa zinazopatikana na kuongeza kipato kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.
Katika hatua nyingine, Katibu wa CCM Kibaha Mjini, Kalleiya, alisema chama pamoja na jumuiya zake kinaendelea kuwa imara huku kikishirikiana kwa karibu na Serikali katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali.

