Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bw. Asangye Bangu, amesema Bodi inatarajia kuongeza bidhaa nyingine tano katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili kuendelea kuwanufaisha watanzania katika sekta mbalimbali.

Akifungua kikao cha wadau cha kujadili na kupitisha Rasimu ya Mpango Mkakati wa WRRB wa miaka mitano (2026/27–2030/31) pamoja na kupokea maoni kuhusu maboresho ya Kanuni za Stakabadhi za Ghala, kilichofanyika Juni 26, 2026, mjini Morogoro, Bw. Bangu amesema mfumo huo umeendelea kukua kwa kasi na kuleta mafanikio makubwa.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita mfumo huo ulikuwa unahusisha bidhaa mbili pekee, lakini kwa sasa unahusisha bidhaa 18, huku maandalizi yakiendelea kuongeza bidhaa nyingine tano ili kuimarisha uwazi, ushindani wa bei na kuongeza fursa za biashara ya mazao.

Bw. Bangu amebainisha kuwa pamoja na kuwanufaisha wakulima kwa kuwawezesha kuuza mazao yao kwa bei yenye ushindani, mfumo huo umechangia kuongeza mapato ya Serikali na kurahisisha Halmashauri kukusanya mapato yatokanayo na biashara ya mazao.

Aidha, amesema WRRB inaendelea na mazungumzo na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) pamoja na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) ili kuwezesha biashara ya mazao kufanyika kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, hatua itakayoongeza ufanisi na uwazi katika biashara hiyo.

Ameongeza kuwa Bodi itaendelea kuhamasisha matumizi ya mfumo huo kwa kuanzisha njia bunifu zitakazowasaidia wakulima kuepuka kuuza mazao yao mara tu baada ya mavuno, wakati bei zikiwa chini.