NA DENIS MLOWE IRINGA
SERIKALI imewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Iringa kuwa ujenzi wa Barabara ya Mzunguko ya Igumbilo–Kihesa (Iringa Bypass) utaanza tena baada ya kukamilisha malipo kwa mkandarasi, hatua inayolenga kuondoa kusuasua kwa mradi huo na kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
Ahadi hiyo ilitolewa bungeni na Naibu Waziri wizara ya ujenzi Injinia Godfrey Kasekenya alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, ambaye alitaka Serikali kueleza lini ujenzi wa mradi huo utaendelea baada ya kusimama kwa muda mrefu.
Ngajilo alisema Serikali tayari ilitoa shilingi bilioni sita kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 41.3, lakini mkandarasi bado anaidai Serikali zaidi ya shilingi bilioni tisa, hali iliyosababisha shughuli za ujenzi kusimama na ajira nyingi za vijana zilizokuwa zimezalishwa kupitia mradi huo kupotea.
Alieleza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya Iringa, hivyo wananchi wanahitaji kufahamu msimamo wa Serikali kuhusu kuendelea kwa utekelezaji wake.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri alisema Serikali inautambua umuhimu wa Iringa Bypass na kwamba aliutembelea mradi huo pamoja na aliyekuwa waziri mkuu awamu iliyopita Kassim Majaliwa wakati wa ziara yake mkoani Iringa, ambapo walijionea hali halisi ya utekelezaji wake.
Alisema barabara hiyo ni ya kimkakati kwa kuwa itakuwa njia mbadala ya usafiri endapo kutatokea changamoto kwenye barabara kuu inayounganisha Iringa na mikoa ya kusini, hivyo Serikali imeipa kipaumbele miongoni mwa miradi iliyokwama ambayo itaanza kutekelezwa baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa inayoendelea kwa sasa.
Naibu Waziri alisisitiza kuwa Serikali ina mpango wa kumlipa mkandarasi ili arejee eneo la mradi na kuendelea na ujenzi kwa haraka, hatua inayotarajiwa kurejesha ajira, kuharakisha utekelezaji wa mradi na kuboresha miundombinu ya usafiri katika Mkoa wa Iringa.
