Na Mwandishi Wetu
WATOA huduma za saluni nchini wametajwa kuwa kundi lenye uwezo mkubwa wa kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kutokana na mwingiliano wao wa karibu na jamii, hali inayowafanya kuwa mabalozi muhimu wa mabadiliko ya tabia na mtazamo kuhusu matumizi ya nishati hiyo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Kidoti Foundation, Jokate Mwegelo, ambaye pia ni mlezi wa Chama cha Salunisti Tanzania (CCST) wakati wa hafla ya kusaini makubaliano ya ushirikiano kati ya Kidoti Foundation na Kampuni ya Oryx Energies Tanzania yenye lengo la kuwawezesha watoa huduma za saluni kutumia nishati safi na kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi yake katika jamii.
“Kundi la wasusi na watoa huduma za saluni lina nafasi ya kipekee kwa kuwa hukutana na mamia ya wananchi kila siku, jambo linaloweza kutumiwa kueneza elimu kuhusu manufaa ya nishati safi ya kupikia kwa urahisi kuliko kutegemea kampeni za kawaida pekee.
“Watoa huduma za saluni wanazungumza na watu wa makundi mbalimbali kila siku. Wanajenga mahusiano ya karibu na wateja wao, hivyo wana nafasi kubwa ya kubadilisha mitazamo kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia. Tunataka wawe mabalozi wa mabadiliko hayo,” amesema.
Ameongeza juhudi za kuhakikisha Watanzania wengi wanatumia nishati safi haziwezi kuachiwa Serikali pekee, bali zinahitaji ushiriki wa makundi yenye ushawishi wa moja kwa moja katika jamii.
Jokate amesema kwamba kupitia ushirikiano huo, watoa huduma za saluni watanufaika kwa kutumia nishati safi katika shughuli zao za kila siku, huku wakipata nafasi ya kuwahamasisha wateja wao kuachana na matumizi ya nishati zinazochafua mazingira na kuhatarisha afya.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Meneja Mauzo wa Oryx Tanzania Shaban Fundi amesema kampuni hiyo imeamua kushirikiana na Kidoti Foundation kwa kutambua kuwa makundi ya kijamii yenye ushawishi yanaweza kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi nchini.
Amesema mbali na kutoa suluhisho la nishati safi, kampuni hiyo inalenga kujenga uelewa wa wananchi kuhusu faida za matumizi ya gesi na teknolojia nyingine za kisasa zinazochangia kulinda afya na mazingira.
“Oryx Gas kwa muda mrefu tumekuwa na mkakati Maalum wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na tumeyafikia makundi mbalimbali na leo hii tumesaini mkataba wa miaka mitatu na Kidoti Foundation ambako sasa tunakwenda kwa kundi muhimu la watoa huduma za saluni.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCST Ntuli Mwakatobe amesema amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu ya kuwawezesha wanachama wa chama hicho kuwa sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya nishati safi nchini.
Amesema wasusi na wamiliki wa saluni wamekuwa wakitafuta njia za kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara zao huku wakihakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama zaidi.
“Leo tunapata nafasi ya kutumia nishati safi lakini pia kuwa sauti ya kuelimisha jamii. Hii ni fursa ambayo tutaenda kuitumia kuwafikia wateja wetu kila siku,” amesema.
Matumizi ya nishati safi ya kupikia yanatajwa kuchangia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa unaochochea mabadiliko ya tabianchi, sambamba na kuboresha maisha ya wanawake ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakibeba mzigo mkubwa wa shughuli za kupikia.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kuwa mwanzo wa ushirikiano mpana utakaowezesha watoa huduma za saluni kuwa sehemu ya mtandao wa mabalozi wa nishati safi nchini, huku wakitumia nafasi yao ya kila siku kuwafikia wananchi wengi zaidi.

